Akizungumza katika Mkutano huo, unaofanyika sanjari na Mkutano wa Muungano wa Afrika, amesifu dhamira ya Italia kupitia Mpango wa Mattei, akiuita “mfano wa kuigwa.”

Guterres amesema “Katika dunia yenye migawanyiko inayoongezeka, mkutano huu unatuma ujumbe ulio wazi. Ujumbe kwamba ushirikiano lazima ujengwe juu ya heshima na uaminifu wa pande zote. Ujumbe kwamba ubia lazima ulenge kutekeleza Ajenda ya 2030 na Ajenda 2063 ya Muungano wa Afrika”.

Kuziba pengo la ufadhili

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amebainisha vipaumbele vitatu vikuu, akianzia na haki ya kifedha.

Ameonya kuwa “Nchi zinazoendelea zinakabiliwa na pengo la ufadhili la dola trilioni 4 kila mwaka kwa ajili ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs). Na nchi za Afrika hulipa hadi mara nane zaidi kukopa kuliko nchi zilizoendelea. Hali hii inakwamisha uwekezaji na fursa”.

Amesisitiza kuwa “Ahadi ya Seville” inatoa ramani ya kuziba pengo la malengo ya Maendeleo endelevu SDGs, kushughulikia changamoto za madeni na kurekebisha mfumo wa kifedha wa kimataifa ili “uendane na hali halisi ya leo, si miundo ya nguvu ya jana.”

“Tunahitaji benki za maendeleo za kimataifa zenye nguvu zaidi, mikopo ya muda mrefu yenye gharama nafuu na suluhu za madeni zinazopunguza hatari na gharama,” amesisitiza, akiongeza kuwa juhudi hizo ni “moja ya njia bora zaidi za kushughulikia mizizi ya uhamiaji usio wa kawaida kwa kuunda ajira, kuimarisha huduma na kurejesha matumaini.”

Kupunguza ongezeko la joto hadi nyuzi joto 1.5°C

Kuhusu mabadiliko ya tabianchi, Katibu Mkuu ameonya kuwa “dunia itazidi nyuzi joto 1.5 C. Lazima tufanye ongezeko hili liwe dogo kadri iwezekanavyo, la muda mfupi na salama.”

Amesisitiza uwezo wa bara la Afrika katika nishati jadidifu na vijana wake wenye nguvu, akieleza kuwa mpito wa nishati unaweza kuwa “kichocheo cha pamoja cha ukuaji.”

“Hata hivyo, Afrika inapokea asilimia mbili tu ya uwekezaji wa kimataifa katika nishati safi. Hili lazima libadilike. Tunahitaji uwekezaji mkubwa katika nishati jadidifu, gridi na hifadhi, kuongezwa kwa ufadhili wa kukabiliana na athari za tabianchi na mifumo ya tahadhari ya mapema inayookoa maisha,” amesema Guterres

Kwa mujibu wake, hili linamaanisha kuhamasisha “dola trilioni 1.3 kwa mwaka kwa nchi zinazoendelea ifikapo 2035,” pamoja na kuhakikisha “minyororo ya thamani iliyo ya haki kwa madini muhimu huku manufaa yakinufaisha wananchi wa Afrika.”

Akili Mnemba AI, salama, wazi na ya haki

Kuhusu mageuzi ya kidijitali, Bwana. Guterres ametangaza kuwa amewasilisha kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa majina ya wataalam 40 kuunda jopo huru la kimataifa la kisayansi kuhusu akili Mnemba (AI), ambapo ripoti yake ya kwanza itasaidia mjadala wa kimataifa kuhusu usimamizi wa AI mwezi Julai.

“Lazima tuhahakikishe kuwa AI ni salama, wazi na ya haki huku manufaa yake yakigawanywa kwa wote. Ndiyo maana ninatoa wito wa kuundwa kwa Mfuko wa Kimataifa wa AI ili kuimarisha uwezo wa msingi kila mahali, ujuzi, data na uwezo nafuu wa kompyuta,” amesema.

Kwa kuhitimisha, amesisitiza kuwa “mafanikio ya Afrika ni muhimu kwa dunia iliyo salama zaidi, yenye usawa zaidi na endelevu zaidi,” akitoa wito kwa Mkutano huo kubadili kanuni za pamoja kuwa “maendeleo na ustawi wa pamoja.”

Mapema leo Katibu Mkuu alikutana na Mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika, Mahmoud Ali Youssouf. Pia amefanya mikutano ya pande mbili na viongozi kadhaa wa Afrika, akiwemo Rais wa Burundi, Évariste Ndayishimiye.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *