Hafla ya utiaji saini wa Hati ya Makubaliano imefanyika jijini Dar es Salaam, Tanzania na kuongozwa na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, Luteni Jenerali Salum Haji Othman.
Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania, Luteni Jenerali Salum Haji Othman (katikati), Mwakilishi wa UN Women Tanzania, Bi Catherine Rose (wa kwanza kushoto), pamoja na wadau kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Makubaliano hayo yanahusu utekelezaji wa mradi wa ‘Measuring Opportunities for Women in Peace Operations’ – MOWIP, unaofadhiliwa na Mfuko wa Elsie Initiative.
Mradi huo unalenga kupima na kuchambua fursa zilizopo kwa wanawake katika operesheni za kulinda amani, pamoja na kubaini changamoto zinazowakabili.
UN Women
Cathetine Rose, Mwakilishi UN Women Tanzania ameshiriki hafla hiyo na anasema, “ushiriki wa wanawake katika operesheni za kulinda amani si suala la usawa pekee, bali ni mkakati unaoongeza ufanisi wa operesheni na mafanikio ya misheni.”
Kupitia mradi huo, tathmini ya kitaifa itafanyika ili kubaini vikwazo na kutoa mapendekezo ya kitaalamu yatakayosaidia kuboresha ajira, mafunzo na mazingira ya kazi kwa wanawake waliopo jeshini.
Baadhi ya maofisa wa Jeshi na Wananchi wa Tanzania wakiwemo maofisa wanawake waliohudhuria hafla ya utiaji saini wa mkataba wa EALSE Initiative Fund kati ya Mkuu wa Chuo cha Ulinzi wa Amani Tanzania nchini DRC.
Ushirikiano huo unatarajiwa kuimarisha zaidi dhamira ya Tanzania katika kutekeleza Ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama, sambamba na Mpango wa Taifa wa Wanawake, Amani na Usalama wa mwaka 2025.
Hatua hii inaelezwa kuwa sehemu ya jitihada za kimkakati za kuhakikisha wanawake wanapata nafasi sawa na kuchangia kikamilifu katika operesheni za kimataifa za kulinda amani.