TANGA: Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba amefichua namna baadhi ya watendaji wa serikali wanavyotumia ujanja kuhalalisha upotevu wa fedha katika miradi.
Dk Mwigulu alieleza hayo jana baada ya kukagua na kufanya uzinduzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kilindi ukiwa ni mwendelezo wa ziara yake iliyoanza juzi mkoani Tanga.
Alisema amebaini katika maeneo mbalimbali watendaji hao wakitumia visingizio vya fedha kutotosha kwa kuongeza gharama za utekelezaji wa miradi na kuomba nyongeza ya fedha kwenye eneo ambalo fedha ingetosha kujenga.
Aliagiza uchunguzi ufanyike kubaini kilichofanyika kusababisha fedha iliyotolewa kujenga hospitali hiyo kukamilisha majengo pungufu na waliohusika kutumia ujanja kuhalalisha upotevu huo wa fedha wakibainika wachukuliwe hatua za kinidhamu na kisheria.
“Kuna michezo naona inaendelea ya kuhalalisha upotevu wa fedha, mfano jana nilipita Handeni Mjini, jambo la VETA kugandisha mifuko ya simenti wakati Tanga kuna viwanda vya simenti eti sementi ya kujenga VETA Tanga imetoka Dar es Salaam ili kuhalalisha gharama za kujenga, tunabebesha serikali mzigo inashindwa kutoa huduma maeneo mengine kwa sababu watu wanapandisha gharama,” alisema.
Aliagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa Tanga kuharakisha upatikanaji wa taarifa kuhusu mradi huo.
“Mnajificha kwenye kichaka cha gharama, mimi nina taarifa zote. Sasa kamanda wa Takukuru fanyia uchunguzi hiki chote kilichofanyika nipate taarifa hiyo nichukue hatua, hatuwezi tukawa na watu mnapindishapindisha habari.
“Halafu fuatilia kila kitu vyote hivi fuatilia hivi vilivyopandisha gharama, hiki kichaka cha gharama fuatilia nipate taarifa na kwamba serikali haiwezi kuvumilia kuwa na watu wanaopindisha ukweli wa mambo ambayo ni ya manufaa ya wananchi,” alisema.
Aliongeza: “Hapa tutajua ni nini kimefanyika, hatuwezi kuwa Rais anahangaika kutafuta fedha halafu watu wa natengeneza vichaka vingine vya kuchelewesha huduma kwa watu, hiyo haikubaliki. Nikija nikagundua na nyinyi mmefanya hivyo kwamba simenti iko Tanga nyie mmeenda kuchukua Mbeya, nondo ziko hapa muende kuchu- kulia Mwanza, nitachukua hatua kali za kinidhamu na za kisheria.”
Awali, Dk Mwigulu alimhoji Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi, Kulwa Mgalula sababu zilizofanya baadhi ya majengo kutokamilika katika hospitali hiyo ambapo alisema walipata fedha ya kujenga majengo tisa lakini gharama za kusafirisha vifaa vya ujenzi zilikuwa kubwa. Alisema waliomba kibali
Tamisemi ili kumalizia majen- go yaliyobaki.
Aidha, Dk Mwigulu aliweka jiwe la msingi la Hos- pitali ya Wilaya ya Kilindi ambapo Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Pendo Mang’ombe alisema ilijengwa kwa gharama ya Sh bilioni 2.64.
Alisema kati ya fedha hizo Sh bilioni 2.51 zimetoka Serikali Kuu na Sh milioni
50 ni za mapato ya ndani ya Halmashauri na Sh milioni 89.9 ni kutoka Benki ya Dunia ambapo ujenzi huo umesaidia kuwapunguzia wananchi adha na gharama kubwa za matibabu na kufuata huduma za afya mbali.
Vilevile, Dk Mwigulu alikagua mradi wa maji wa Kwamaligwa uliopo wilayani Kilindi ambao utagharimu Sh bilioni 6.98 hadi kukamilika kwake.
Alisema mradi huo unata- rajiwa kuhudumia wananchi 36,263, wakiwemo wananchi 32,641 wa Kata ya Kibirashi (vijiji sita) na wananchi 3,622 wa Kata ya Kisangasa, Kijiji cha Kwediswati.
Alisikiliza kero za wananchi wa eneo hilo ikiwa ni pamoja na tatizo la maji katika eneo la Makasini na upungufu wa walimu katika Shule ya Msingi Mgera ambayo ina walimu watatu pekee ambapo aliwataka mawaziri husika katika maeneo yote yaliyolalamikiwa kufuatilia na kuyatafutia ufumbuzi.
