
Sheikh Naim Qassim Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa harakati hiyo ya muqawama haitaki vita lakini imejiandaa kikamilifu kuilinda Lebanon na kutoa jibu kali kwa uchokozi wowote wa maadui wa nchi hiyo.
“Sisi katika Hizbullah hatutaki vita na hatuna lengo la kuanzisha vita lakini kamwe hatutasalimu amri na tuko tayari kuihami nchi,” amesema Katibu Mkuu wa Hizbullah katika hotuba iliyorushwa hewani na televisheni kutoka mji mkuu wa Lebanon, Beirut.
Amesema kuna tofauti kubwa kati ya kukabiliana na uchokozi na kuanzisha vita. “Tuko tayari kuihami Lebabon. Hatutakubali vitisho.”
Sheikh Naim Qassim amesema kuwa maadui hawatofanikiwa mbele ya kundi ya muqawama lenye ari na azma thabiti, bega kwa bega na taifa kubwa na thabiti la Lebanon.
Sheikh Naim Qassim ameongeza kuwa misingi mikuu ni kulinda ardhi ya Lebanon kwa sababu kuilinda nchi ni jukumu la kila mtu.
Amesema, Hizbullah inaunga mkono umoja wa kitaifa wa Lebanon, mamlaka kamili ya kujitawala na kukomboa ardhi ya nchi, na inapinga aina zote za fitina.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah amesema serikali ya Lebanon inabeba dhima kikamilifu kufuatia mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Israel na kwamba mamlaka tawala zinapasa kuwajibika kwa sababu zilisaini makubaliano ya kusitisha mapigano na utawala wa Tel Aviv.