
Simba imetinga raundi ya 32 bora ya Kombe la Shirikisho la CRDB msimu huu baada ya leo kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Greenland katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam.
Mabao ya Simba katika mchezo huo yamefungwa na Baraka Mwangosi, Anthony Mligo na Neo Maema.
Mwangosi alifunga bao la kwanza katika dakika ya 12 na katika dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza, Mligo akaipatia timu take bao la pili.
Wakati mchezo huo ukielekea kumalizika, Neo Maema alipigilia msumari wa mwisho katika jeneza la Greenland baada ya kuifungia Simba bao la tatu.
Katika mchezo mwingine wa mashindano Jay’ı leo, KMC imekuwa timu ya kwanza ya Ligi Kuu Tanzania Bara kuaga mashindano ya Kombe la Shirikisho la CRDB baada ya kufungwa kwa mikwaju ya penalti 3-2 na Bandari Tanzania leo, Jumanne, Februari 17, 2026.
Mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam, ulilazimika kuamriwa kwa mikwaju ya penalti baada ya timu hizo kutoka sare ya mabao 3-3 katika dakika 90 za kawaida.
Bandari Tanzania ni timu inayoshiriki Ligi ya Kwanza (First League) ambayo zamani ilikuwa ikitambulika kama Ligi Daraja la Pili.
Mkoani Mbeya, Mbeya City imejikuta ikisubiria ushindi wa mezani baada ya wapinzani wao Biashara United kutotokea uwanjani katika mchezo uliopangwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Halmashauri Chunya.
Transit Camp imeichabanga Chama la Wana kwa mabao 4-0 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Filbert Bayi na katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, wenyeji Coastal Union wameibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Nyumbu FC.
Dodoma Jiji imepata ushindi wa mabao 3-1 nyumbani katika Uwanja wa Jamhuri Dodoma dhidi ya Kilimanjaro Wonders na Fountain Gate imepata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mapinduzi katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Matokeo ya Mechi za leo Kombe la Shirikisho la CRDB
Coastal Union 3-1 Nyumbu FC
Transit Camp 4-0 Chama la Wana
Dodoma Jiji 3-1 Kilimanjaro Wonders
KMC 3(2)-3(3) Bandari Tanzania
Fountain Gate 1-0 Mapinduzi
Simba 3-0 Greenland