SERIKALI ya Tanzania ipo mbioni kukamilisha hatua za mwisho za kuridhia Mikataba ya kazi namba 189 na 190 ya Shirika la Kazi Duniani (ILO), inayolenga kutambua kazi za ndani kama ajira rasmi zenye staha na ulinzi wa kisheria.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Febuari 18, kwa niaba ya Serikali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi na Uwekezaji Rashidy Ally Salim amesema tayari Serikali imeanza kufanyia kazi vipengele mbalimbali vya mikataba hiyo ikiwemo kuweka viwango stahiki vya mishahara na kuandaa mikataba rasmi ya ajira ili kuhakikisha wafanyakazi wa ndani wanapata hifadhi ya jamii.

Amesema hatua hii itasaidia kuimarisha ulinzi wa wafanyakazi wa ndani dhidi ya unyanyasaji, ukatili na mazingira yasiyo salama ya kazi sambamba na kuongeza hadhi ya sekta hiyo nchini. Aidha, katika mradi wa Employed, mwakilishi wa Ubalozi wa Italia nchini David Lorenzin, mwakilishi wa taasisi ya CVM, Magesa Padre, na Katibu Mkuu wa CHODAWU, Esta Ria wamesema mradi huo umelenga kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa ndani kutoka mikoa tisa nchini.
Mradi huo umegharimu takribani Shilingi bilioni 3.6 na umewezesha zaidi ya wafanyakazi 1,000 kupata mafunzo ya kitaaluma na elimu kuhusu haki zao za msingi kwa lengo la kuwawezesha kutambua kazi yao ni rasmi. Katika hafla ya uzinduzi wa utafiti na matokeo ya utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi huo, mwakilishi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Sara Kisanga, pamoja na mwakilishi wa VETA Tanzania, Andale Ngodi, wamesema mradi huo umeleta mabadiliko chanya ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa mitaala rasmi ya mafunzo.

Mitaala hiyo inalenga kuwaandaa walimu na wataalamu watakaotoa elimu kwa wafanyakazi wa ndani hatua inayolenga kuleta taaluma rasmi na kuongeza heshima ya kazi za ndani nchini. Serikali inasema hatua ya kuridhia mikataba hii ya ILO ni sehemu ya juhudi zake za kuimarisha haki na ustawi wa wafanyakazi sambamba na kutekeleza viwango vya kimataifa vya ajira zenye staha.SOMA: Wasaidizi kazi za ndani wapewa mafunzo