
Sheikh Sadiq al-Ghariani, Mufti wa Libya amesema kwamba kuikomboa Palestina na kuwasaidia wakazi wake ni wajibu wa kidini kwa Waislamu wote.
Al-Ghariani ameongeza kuwa, kuikomboa Baitul-Muqaddas na nchi ya Palestina kutoka katika uvamizi wa utawala wa Kizayuni wa Israel ni wajibu kwa Waislamu wote, na wajibu huu hauwezi kuondolewa kwao isipokuwa kwa kuutimiza.”
Mufti wa Libya amesema kuwa: “Jukumu hili la kidini na kihistoria linawalazimisha watawala na mataifa yote ya Kiislamu kuchukua hatua za haraka na madhubuti za kuwasaidia watetezi wa Baitul-Muqaddas na maeneo yote yanayokaliwa kwa mabavu.”
Mufti Al-Ghariani amesema: “Mauaji ya kimbari ya kupangwa na njaa dhidi ya watu wa Palestina yanahitaji hatua za Umma wa Kiislamu za kuwasaidia, na hatua hizi lazima ziwe zaidi ya kulaani kwa maneno na kutoa kauli za kuchukizwa na jambo hilo.”
Sambamba na kueleza kwamba ulegevu katika kuwasaidia wanaokandamizwa katika hatua hii nyeti na ngumu unatambuliwa kama kushindwa katika kutimiza majukumu ya kidini na kusisitiza kwamba: “Kutoa msaada kamili wa kimwili na kiroho na maandalizi ya kuimarisha muqawama na mapambano ya watu wa Palestina ni jambo muhimu na la dharura.”
Mufti wa Libya amesisitiza zaidi haja ya kuamsha silaha ya vikwazo kamili dhidi ya nchi na makampuni yote yanayouunga mkono utawala wa Kizayuni wa Israel akiitaja kuwa ni Jihadi ya kiuchumi ambayo ni lazima kwa kila Mwislamu.
Al-Ghariani ameongeza: “Suala la Palestina ndilo suala kuu la Umma wa Kiislamu, na ushindi unategemea kuzingatia haki na kutofumbia macho hata kipande kidogo kabisa cha ardhi ya Palestina.” Amemalizia kwa kusifu mapambano ya wakazi wa Ukanda wa Gaza, ambao wametetea heshima na hadhi ya Umma mzima wa Kiislamu na kusimama kidete dhidi ya mashine ya mauaji na uharibifu ya utawala haramu wa Israel.