GEITA: TAKRIBANI vijana 1001 wilayani Geita wamehitimu mafunzo ya ulinzi shirikishi kupitia Programu ya Polisi Jamii mkoani Geita iliyofadhiliwa na Kampuni ya Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML).

Programu hiyo imeratibiwa na kutekelezwa kwa ushirikiano na Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita dhamira kuu ikiwa ni kuimarisha ulinzi na usalama kupitia ushirikishaji wa vijana katika jamii.

Akizungumza katika hafla ya kufunga mafunzo, Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Ashraf Suryaningrat amesema ufadhili huo unakuja kwa kutambua kuwa usalama ni mchakato shirikishi.

Amesema GGML inaunga mkono ulinzi shirikishi kwani usalama wa kweli hupatikana pale ambapo jamii, vyombo vya dola na wadau wengine wanashirikiana kwa lengo moja la pamoja.

Amesema programu hiyo imebuniwa kuwawezesha wananchi kuwa washiriki hai katika kudumisha amani, kuhamasisha uzingatiaji wa sheria na kusaidia kuzuia uhalifu kabla haujatokea.

Naye Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Safia Jongo amesema programu hiyo inalenga kudumisha usalama, amani na utulivu mkoani humo.

Amesema utekelezaji wa programu hiyo ulianza rasmi mwaka 2016 ambapo mifumo ya ulinzi imeimarika kwa kuunda na kuhuisha vikundi vya ulinzi shirikishi chini ya serikali za mitaa.

Amesema kwa mwaka 2026 mafunzo hayo yamejumuisha vijana kutoka kata saba za wilaya ya Geita sambamba na mitaa saba na vijiji 10 inayozunguka mgodi wa GGML.

Kamanda Jongo amewataka vijana kuhakikisha mafunzo hayo yakawe chachu ya mabadiliko kwa kuyatumia kikamirifu kuleta matokeo chanya kwa ushirikiano na viongozi wa serikali za mitaa.

Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mkuu wa wilaya ya Chato Louis Bura ameagiza programu ya polisi jamii itekelezwe kwa ufasaha kufanikisha ajenda ya kuimarisha amani ya katika mkoa.

Bura amesisitiza kuwa ushiriki wa vijana mkoani Geita kwenye programu hiyo ni muhimu katika kuunga mkono juhudi zinazoendelea kufanywa na serikali kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *