Mjumbe mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya ameonya Jumatano kuwa kuongezeka kwa mgawanyiko ndani ya mfumo wa mahakama wa nchi hiyo, pamoja na kuzorota kwa hali ya uchumi, kunatishia umoja wa kitaifa na kunaweza kuyumbisha uthabiti wa eneo zima.

Hanna Tetteh ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba, “hali nchini Libya inazidi kudorora katika nyanja nyingi.”

Tetteh amesema kuwa mfumo wa mahakama wa Libya, ambao kihistoria umeendelea kubaki kwa kiasi kikubwa katika umoja licha ya changamoto za muda mrefu za kisiasa, ikiwemo Mahakama ya Juu ya Tripoli na Baraza lake la Kikatiba kama chombo cha juu zaidi cha kikatiba,sasa unazidi kugawanyika, jambo lenye athari kubwa kwa umoja wa nchi.

Alionya kuwa kuwepo kwa maamuzi ya kisheria yanayokinzana kutadhoofisha utawala bora na kuzorotesha juhudi zinazoendelea za Umoja wa Mataifa za kuwezesha mchakato wa kisiasa.

Tetteh amesisitiza kuwa: “Iwapo hatua hazitachukuliwa kulinda umoja, mshikamano na uhuru wa mahakama, mifumo ya kisheria inayokinzana itayoibuka itaathiri uchumi, uchaguzi, utawala, usalama na haki za binadamu. Huu ni mstari mwekundu ambao ukivukwa unaweza kudhoofisha umoja wa dola.”

Amewasihi viongozi wa Libya kujiepusha na hatua za kuchochea mivutano na kushirikiana na kamati huru ya upatanishi ya Walibya, inayoundwa na wataalamu wa sheria na mahakama, inayolenga kudumisha umoja wa mfumo wa mahakama.

Zaidi ya migawanyiko ya kitaasisi, Tetteh ameangazia hali mbaya ya uchumi wa Libya, akitaja kushuka kwa thamani ya sarafu, kupanda kwa bei za bidhaa, uhaba wa mafuta, na kuongezeka kwa hali ya kukata tamaa miongoni mwa wananchi.

Alionya zaidi kuwa kuzorota kwa hali ya uchumi, kunapounganishwa na mazingira dhaifu ya kiusalama, kunaweza kusababisha migogoro ya kisiasa na kiusalama isiyotabirika.

Libya imekumbwa na vurugu na machafuko tangu kuondolewa madarakani na kuuawa kwa kiongozi wake wa muda mrefu, Muammar Gaddafi, kufuatia mashambulizi ya anga yaliyoongozwa na muungano wa kijeshi wa NATO chini ya uongozi wa Marekani mwaka 2011. Machafuko yaliyofuatia na migawanyiko ya makundi yaligeuka kuwa vita vya uwakala wa kikanda, vilivyochochewa na mataifa ya nje yaliyomiminia nchi hiyo silaha na wapiganaji wa kulipwa.

Tangu mwaka 2015, Libya imegawanyika kati ya Serikali ya Maridhiano ya Kitaifa (GNA) inayotambuliwa kimataifa yenye makao yake Tripoli, na wabunge walioko Tobruk wanaoungwa mkono na kamanda wa kijeshi aliyeasi, Khalifa Haftar.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *