MPANGO wa kuanzisha mfuko wa kitaifa wa miundombinu nchini Kenya umekumbwa na changamoto mbalimbali ambazo zimezua mjadala mkubwa kuhusu mustakabali wa uchumi wa nchi hiyo hasa wakati taifa hilo likijiandaa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Kwa sasa, hali ya uchumi inaonekana kuwa na presha ikilinganishwa na miaka iliyopita hali inayochangiwa na maamuzi ya sera pamoja na mazingira ya kifedha yanayobadilika. Mfuko huo uliopendekezwa chini ya uongozi wa Rais William Ruto ulikusudiwa kusaidia kufadhili miradi mikubwa ya miundombinu na kuvutia uwekezaji wa muda mrefu.
Hata hivyo, kabla haujaanza kufanya kazi kikamilifu tayari umekumbwa na changamoto za kisheria na kiutawala ambazo zimezuia utekelezaji wake.Baada ya Baraza la Mawaziri kuidhinisha kuanzishwa kwake Desemba 2025 Mahakama Kuu ya Kenya ilitoa amri ya kusimamisha utekelezaji wake kwa muda ikieleza kuwa mfuko huo uliundwa bila kupitishwa na Bunge.

Hatahivyo uamuzi huo umeibua maswali kuhusu uwazi, usimamizi wa fedha za umma na uhalali wa mpango huo. Mbali na changamoto za kisheria pia kuna upungufu wa imani kutoka kwa wawekezaji, wanasiasa na wananchi. Wadau wengi wanaona kuwa muundo uliopendekezwa wa mfuko huo uliowekwa kama kampuni badala ya mfuko wa umma unaosimamiwa kisheria, unaoweza kupunguza usimamizi wa Bunge na kuongeza hatari ya matumizi yasiyo wazi ya fedha.
Hali hii imeathiri imani ya wawekezaji wa ndani na wa kimataifa ambao wangetarajiwa kushiriki katika miradi ya miundombinu. Aidha Kenya imekuwa na changamoto za muda mrefu katika kuandaa miradi ya miundombinu ambayo inaweza kuvutia uwekezaji mkubwa. Miradi mingi hukosa maandalizi ya kutosha kama tafiti za kina za uwezekano, mifumo ya mapato iliyo wazi na mipango ya kupunguza hatari kwa wawekezaji.
Bila miradi iliyoandaliwa vizuri, mfuko kama huu huwa na ugumu wa kuvutia fedha kutoka kwa taasisi za kifedha, mifuko ya pensheni na wawekezaji wa kimataifa. Deni la taifa limekuwa likiongezeka na gharama za kulihudumia zinapunguza uwezo wa serikali kufadhili miradi mipya. Hali hii pia inawafanya wawekezaji kuwa waangalifu zaidi kuwekeza katika miradi mikubwa inayohusisha serikali.

Hata hivyo, wataalamu wa uchumi wanaamini kuwa wazo la mfuko wa miundombinu si baya bali changamoto zake zinatokana na ukosefu wa misingi imara ya kisheria, mifumo thabiti ya uongozi na miradi iliyo tayari kwa uwekezaji. Nchi nyingine duniani zimefanikiwa kuanzisha mifuko kama hiyo kwa kuweka sheria wazi, usimamizi wa kitaalamu na kuhakikisha miradi ina faida na inaweza kulipa wawekezaji.
Kwa hiyo, ili mpango huo ufanikiwe, Kenya inahitaji kujenga upya imani kwa wawekezaji na wananchi, kuweka mfumo wa kisheria ulio wazi na kuandaa miradi yenye tija inayoweza kuvutia mitaji ya muda mrefu. Bila kufanya hivyo, mfuko wa miundombinu unaweza kuendelea kubaki kuwa wazo zuri lisiloweza kutekelezwa kikamilifu, badala ya kuwa chombo muhimu cha maendeleo ya nchi.