
Msemaji wa ikulu ya White House Karoline Leavitt ametangaza kuwa rais wa Marekani Donald Trump anatazamiwa kufanya mkutano na viongozi wa nchi za Kiarabu na Kiislamu kujadili kadhia ya Ghaza.
Ikimnukuu Leavitt, tovuti ya habari ya Axios imesema, Trump atakutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Saudi Arabia, Muungano wa Falme za Kiarabu UAE, Qatar, Misri, Jordan, Uturuki, Indonesia na Pakistan.
Ikimnukuu mtu mwenye uelewa wa kadhia hiyo, Axios imeongeza kuwa, Trump atawasilisha kwa jopo la nchi hizo pendekezo la mpango wa amani na mfumo wa utawala wa baada ya vita huko Ghaza.
Tovuti hiyo ya habari imebainisha kuwa, mbali na suala la kuachiliwa huru mateka na kukomeshwa vita, Trump anatarajiwa kujadili mipango ya Marekani kuhusiana na kuondoka jeshi la utawala wa kizayuni wa Israel na utawala utakaoiendesha Ghaza baada ya vita bila ya kusihirikisha harakati ya ukombozi wa Palestina ya Hamas.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Washington itazitaka nchi za Kiarabu na Kiislamu zikubali kutuma vikosi vya kijeshi huko Ghaza ili kuwezesha majeshi vamizi ya Israel kuondoka katika eneo hilo na kufadhili kifedha pia shughuli za mpito na ujengaji mpya wa Ghaza.
Hayo yanajiri baada ya viongozi wa nchi sita, ikiwa ni pamoja na Ufaransa, kuamua kuitambua Palestina kama nchi-dola katika mkutano wa ngazi ya juu wa suluhu ya nchi mbili uliofanyika kabla ya mkutano wa kila mwaka wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) huko New York.
Inafaa kuashiria hapa kuwa, tangu Oktoba 2023 hadi sasa, jeshi la utawala wa kizayuni limeshawaua shahidi Wapalestina wapatao 65,344 huko Ghaza, wengi wao wakiwa wanawake na watoto. Mashambulio hayo ya kinyama na ya mtawalia yamelifanya eneo hilo lisiweze kukalika na kusababisha baa la njaa na mripuko wa magonjwa mbalimbali…/