Afrika Kusini imewarejesha nyumbani wageni 2,745 katika wiki moja baada ya Rais Cyril Ramaphosa kuapa kuchukua hatua kali dhidi ya uhamiaji haramu.

Afrika Kusini, moja ya nchi zenye uchumi mkubwa barani Afrika, kwa muda mrefu imekuwa ikiwavutia wafanyakazi wahamiaji kutoka kote barani Afrika, kisheria na kinyume cha sheria.

Lakini sasa nchi hiyo yenye zaidi ya asilimia 30 ya kiwango cha ukosefu wa ajira, imeshuhudia milipuko ya mara kwa mara ya machafuko dhidi ya wahamiaji, ikiwa ni pamoja na vurugu mpya zilizotokea katika wiki za hivi karibuni.

Umati wa Waafrika Kusini wakiwa wamebeba fimbo, mijeledi na ngao wamekuwa wakiandamana katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo wakiwaamuru wageni wasio na hati za ukaazi kuondoka nchini humo hadi kufikia Juni 30.

Hofu inayoongezeka ya usalama baada ya biashara za wahamiaji kuporwa na wageni kushambuliwa, imewafanya raia wa Nigeria, Malawi, Ghana, Zimbabwe na Msumbiji kukubali kurejeshwa nyumbani kwa hiari katika operesheni iliyoandaliwa na serikali za nchi zao.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Afrika Kusini, Leon Schreiber amewaambia waandishi wa habari kwamba: “Kufikia jana usiku, idadi tunayoweza kuripoti ni watu 2,745 waliorejeshwa makwao.”

Serikali ya Afrika Kusini imesema wengi kati ya waliorudishwa makwao walikuwa nchini humo kinyume cha sheria.

Idadi hiyo inajumuisha raia wa Malawi, ambapo takriban 7,000 kati yao wamekuwa wakihifadhiwa katika eneo la wazi katika mji wa bandari wa mashariki wa Durban. Haya ni kwa mujibu wa kamati ya uhamiaji ya wizara mbalimbali iliyoundwa baada ya Rais Cyril Ramaphosa kuapa kuchukua hatua kali dhidi ya uhamiaji haramu.

“Nimefarijika kwamba hatimaye tunaondoka. Ni bora kuliko kuishi hapa kwa hofu,” amesema Fortunate Chilenje kutoka Blantyre, mji mkuu wa kibiashara wa Malawi.

Kwa mujibu wa Shirika la Takwimu la Afrika kusini, zaidi ya wageni milioni tatu wanaoishi nchini humo, ambao ni sawa na asilimia 5.1 ya idadi ya watu wa nchi hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *