Mkuu wa Idara ya Masuala ya Siasa na Ujenzi wa Amani, Rosemary DiCarlo, ametoa kauli hiyo wakati Baraza lilipokutana alasiri ya Jumatano Februari 18 jijini New York, Marekani katika kikao cha kawaida kujadili hali ya Mashariki ya Kati hususan suala la Palestina.
“Juhudi za sasa zinapaswa kulenga kuimarisha usitishaji huo wa mapigano, kuongeza misaada ya kibinadamu na kuweka msingi wa amani ya kudumu kwa kuzingatia sheria za kimataifa,” amesema Bi. DiCarlo.
Rosemary DiCarlo, Mkuu wa Idara ya Umoja wa Mataifa ya Siasa na Ujenzi wa Amani, akizungumza jijini New York, Marekani wakati wa mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu hali katika Mashariki ya Kati, ikiwa ni pamoja na suala la Palestina.
Amegusia mkutano wa kesho wa Bodi ya Amani utakaofanyika Washington, D.C, mji mkuu wa Marekani akisema kuwa, “mkutano huo ni hatua muhimu katika kutekeleza awamu ya pili ya makubaliano ya Gaza na kufufua mchakato wa kisiasa kuelekea suluhisho la uwepo wa mataifa mawili, yaani Israeli na Palestina.”
Ameeleza kuwa hatua hiyo inapaswa kujumuisha kuondolewa kwa silaha Gaza, kusambaratishwa kwa silaha za Hamas na makundi mengine yenye silaha, pamoja na kuweka utaratibu wa usalama na uongozi wa mpito.
Mpango unaoongozwa na Marekani utekelezwe
Hata hivyo, DiCarlo ameonya kuwa mashambulizi ya hivi karibuni ya kijeshi yameua makumi ya wapalestina, wakiwemo wanawake na watoto, huku hali katika Ukingo wa Magharibi ikiendelea kuzorota kutokana na operesheni za kijeshi, upanuzi wa makazi ya walowezi na ubomoaji wa nyumba.
Amesisitiza kuwa njia pekee ya kusonga mbele ni utekelezaji kamili wa mpango wa amani unaoongozwa na Marekani, kuongeza misaada kwa Gaza, kusitisha hatua za upande mmoja na kurejesha mwelekeo wa kisiasa unaoaminika utakaomaliza mzozo na kuleta suluhisho la mataifa mawili kwa mujibu wa maazimio ya Umoja wa Mataifa.
Gaza haitofanikiwa iwapo Ukingo wa Magharibi utaanguka – Qasas
Hiba Qasas amehutubia Baraza kama mpalestina aliyekulia Ukingo wa Magharibi, na kama mwanzilishi wa Wakfu wa Kanuni za Amani ambapo amesema, “tunaanza na ukweli mmoja,” amesema. “Hali ilivyo sasa haiwezi kuendelea kwa pande zote mbili; hakuna upande unaoweza kupata usalama wa kudumu, utu na ustawi kwa gharama ya mwingine.”
Hiba Qasas wa Muasisi na Mkurugenzi Mtendaji wa Wakfu wa Kanuni za Amani, akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu hali katika Mashariki ya Kati.
Amesema awamu ya pili itadumu tu ikiwa uokoaji wa Gaza hautatenganishwa na Ukingo wa Magharibi – ukiwa umeunganishwa kimkakati, ukilindwa kwa dhamana madhubuti na kuongozwa na mwelekeo wa kisiasa ulio wazi na wenye muda maalum.
“Gaza haiwezi kufanikiwa ikiwa Ukingo wa Magharibi utaanguka,” amesema Bi. Qasas.
Fursa ya sasa si ya kuikosa – Tamir
Wajumbe pia wamehutubiwa na Nadav Tamir ambaye ni mzayuni na pia mwanachama wa wa muungano wa United for a Shared Future, yaani Muungano kwa Mustakabali wa Pamoja unaowakutanisha takriban viongozi 550 wa Israeli na Palestina kutoka sekta za usalama, siasa, biashara, asasi za kiraia na vyombo vya habari
Amesema licha ya maumivu na mshtuko uliowapata watu wa pande zote mbili kufuatia mauaji ya tarehe 7 Oktoba 2023, “wakati huu unatoa fursa ya kihistoria ambayo haipaswi kukosa.”
Tamir amesema hali inayoongezeka ya dharura – ndani ya jumuiya ya kimataifa na kote Mashariki ya Kati – inapaswa kutafsiriwa kuwa “njia iliyo wazi na isiyoweza kurudishwa nyuma” kuelekea kuanzishwa kwa Taifa la Palestina lisilo na silaha sambamba na Israel, likiwa limejikita katika muungano wa kikanda.
Ameeleza maono hayo kama “suluhisho la mataifa 23”: Israel, Palestina na mataifa 21 ya kiarabu yaliyoidhinisha Mpango wa Amani wa Kiarabu na kuhalalisha uhusiano wa kidiplomasia.
Kauli za baadhi ya wajumbe wa Baraza
Uingereza ambayo inashikilia Urais wa Baraza la Usalama mwezi huu wa Februari, imewakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Masuala ya Maendeleo, Yvetter Cooper ambaye amesema, “Hamas wapokonywe silaha na wasiwe na siku zijazo wasiwe na dhima yoyote ya uendeshaji wa Gaza.
Mohammad Ishaq Dar, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistani amesema taifa hilo la Asia linashiriki kikamilifu kwenye juhudi za kidiplomasia zenye lengo la sitisho la uhasama na suluhu la haki kwenye mzozo unaoendelea.
Mwakilishi wa Kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Mike Waltz ametumia hotuba yake kusihi wadau wote kuunga mkono Bodi ya Amani iliyoanzishwa kupitia azimio la Baraza namba 2803 la mwaka 2025 akisema “kesho Bodi itatangaza Ahadi ya dola bilioni 5 kwa ajili ya ujenzi mpya wa Gaza.”
Somalia imetoa kauli kupitia Mwakilishi wake wa Kudumu kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Abukar Dahir Osman ambaye amesema, “jamii ya kimataifa lazima ishikamane dhidi ya jaribio lolote la kubadili kinguvu au kijeshi demografia ya maeneo ya wapalestina.”
Palestina itasalia mali ya wapalestina – Mansour
“Hakuna amani popote, wakati wowote,” amesema Riyad Mansour, Mwangalizi wa Kudumu wa Palestina kwenye Umoja wa Mataifa, akihutubia wajumbe huku akieleza uharibifu wa nyumba za ibada za kikristo na kiislamu zenye historia ya karne nyingi, pamoja na vizuizi vya kijeshi na masharti yanayowazuia waislamu na wakristo kutekeleza hija zao.
Amesema lengo la Israeli ni kuwaondoa wapalestina na kutwaa ardhi yao, na kwamba ingawa ukubwa na kasi ya hatua hizo zimebadilika kwa kiasi kikubwa, mbinu na malengo yamebaki yale yale: makazi ya walowezi, ugaidi unaofanywa na walowezi, unyakuzi wa ardhi, ubomoaji wa nyumba na udhibiti wa usajili wa ardhi — yote yakilenga kufanikisha lengo la mwisho la kujigemea eneo.
“Palestina ni mali ya watu wa Palestina,” amesisitiza akiongeza kuwa, “si kitu cha kugawanywa wala si cha kuuzwa.” Licha ya juhudi hizo, amesema, “Israel haitatufanya kuwa watu wasio na ardhi.”
Balozi Mansour amesema “kwa hakika, hatua za kutwaa ardhi zinaendelea waziwazi, na zisipopatiwa upinzani, zitaamua na kuangamiza mustakabali wa eneo hilo.”
Katu Israeli haitotelekeza urithi wake – Saar
Ukawadia wakati wa Gideon Saar, Waziri wa Mambo ya Nje wa Israeli, kuhutubia Baraza ambaye amesema ni “jambo la kuchekesha” kumsikia Mwakilishi wa Kudumu wa Urusi akizungumzia sheria za kimataifa, uvamizi, upanuzi wa ardhi na suluhu ya amani.
Amesema uwepo wa wayahudi katika Israel, hata katika kipindi chote cha uhamisho wa muda mrefu, haujawahi kukoma. “Huenda hiki ndiyo kisa kilicho wazi zaidi na chenye ushahidi wa kihistoria kuliko visa vyote kuhusu haki ya taifa kwa ardhi yake,” amesema.
Saar katika hotuba yake ametumia vielelezo. Mathalani akiinua kishikio cha mtungi kutoka Ufalme wa Yudea kilichopatikana na chenye umri wa miaka 2,700, pamoja na sarafu ya zaidi ya miaka 2,000 iliyogunduliwa katika Jangwa la Yudea wakati wa uasi wa wayahudi dhidi ya warumi, amehoji: “Inawezekanaje uwepo wa wayahudi katika ardhi yetu ya mababu uvunje sheria za kimataifa?”
Pia ameonesha ramani ya enzi ya Uingereza kusimamia dola, akisisitiza kuwa Azimio la Balfour lilirejesha wazo la kuwa na makazi ya kitaifa ya wayahudi katika ardhi yao. “Hatutasaliti urithi wetu, usalama wetu na mustakabali wetu kwa sababu ya changamoto za kisiasa za ndani za mataifa mengine,” amesema.