MOROGORO: NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma, amesema TCB Selous Marathon iliyofanyika kwa msimu wa saba katika mkoa wa Morogoro inaunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita ya kuhamasisha mazoezi, kuimarisha afya za wananchi na kuleta mshikamano wa kijamii.
Mwinjuma amesema hayo wakati akikabidhi baadhi ya zawadi kwa washiriki na kuhitimisha msimu wa saba wa TCB Selous Marathon katika uwanja wa Jamhuri Juni 20,2026 mjini Morogoro.

Naibu Waziri amesema Serikali imekuwa inatoa fedha nyingi kutibia wananchi wake ambalo ni jukumu lake la kimsingi na kwamba magonjwa mwengine yanaweza kuzuirika endapo wananchi watashiriki shughuli za kufanya mazoezi kama hayo ya TCB Selous Marathon ikiwa na kutengeneza mahusiano .
Amesema marathon hiyo imeendelea kukua kila mwaka na kutoa fursa kwa makundi yote ya jamii, ikiwemo watu wenye ulemavu, kushiriki katika shughuli za michezo na kujenga umoja wa Watanzania.
“ Ninaamini mwakani (2027) tutakuwa na TCB Selous Marathon nzuri zaidi na sisi tuliopewa dhamana ya Mheshimiwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan ya kusimamia sekta mbalimbai ikiwemo hii ya michezo , tunawafurahia na mnafanya kazi yetu iwe rahisi,” amesema Mwinjuma.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TCB, Adam Mihayo, amesema udhamini wa benki hiyo katika marathon hiyo unalenga kuboresha afya, kukuza utalii, utunzaji wa mazingira na fursa za kiuchumi.
Amesema kuwa marathon hiyo imesaidia kutangaza mradi wa kimkakati wa Reli ya Kisasa ya (SGR) na vivutio vya utalii vya Tanzania kwa wageni kutoka ndani na nje ya nchi.
Mihayo amesema marathon hiyo imeweka rekodi mpya baada ya kuvutia zaidi ya washiriki 10,000, jambo lililoifanya kuwa mojawapo ya matukio makubwa zaidi ya michezo mkoani Morogoro.

“ Idadi kubwa hii imechochea shughuli za kiuchumi mkoani Morogoro kwenye sekta za hoteli, usafiri, biashara ndogo na huduma mbalimbali zikiongeza mapato kutokana na ongezeko la wageni na pia imehamaisha matumizi ya mifumo ya malipo ya kidijitali” amesema Mihayo.
Mihayo amesema kupitia tukio hilo, TCB inalenga kutangaza Hifadhi ya Selous katika kuunga mkono juhudi za upandaji miti ambapo miti 2,000 tayari imepandwa na mingine 8,000 itapandwa na kufanya jumla kufikia miti 10,000 ikiwa ni hatua ya utunzaji wa mazingira.

Mmoja wa washiriki, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Uwekezaji na Huduma za Wawekezaji Tanzania (UTT AMIS) ,Profesa Faustin Kamuzora aliyeshiriki mbio za kilometa 10 ametoa wito kwa wananchi kujenga tabia ya kufanya mazoezi ya mara kwa mara ili kuboresha afya zao.
“ Suala la afya ni mtaji mkuu na haiji bila ya mwanadamu kujibidiisha kufanya mazoezi ya mara kwa mara ,hata sayansi ipo wazi kuwa kadiri tunavyojibiiidha miili yetu tunaboresha ule mmeng’enyo wa chakula na kuuweka sawa “ amesema Profesa Kamuzora .
Profesa Kamuzora ametumia fursa hiyo kuwashauri viongozi wawe mfano kushiriki kufanya mazoezi ili kuboresha afya zao na kuwa mfano kwa watumishi waliochini yao.