
Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiwa na mkakati wa kuwezesha sekta ya uvuvi kufikia kuchangia asilimia 10 ya Pato la Taifa (GDP) ifikapo 2030, wadau waeleza mbinu zitakazosaidia kufanikisha hilo.
Hadi sasa sekta ya uvuvi inatajwa kuchangia asilimia 1.8 ya pato la Taifa huku wadau wakisisitiza uwekezaji zaidi katika teknolojia, utoaji wa mikopo, elimu pamoja na ukuzaji wa soko la samaki na vyakula vya majini.
Hayo yameelezwa na wadau leo Alhamisi, Februari 19, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa warsha ya kitaifa kuhusu uundaji wa nadharia ya mabadiliko kwa mageuzi ya mifumo ya vyakula vya majini Tanzania, iliyowakutanisha watafiti, watunga sera na washirika wa maendeleo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika warsha hiyo, Mtafiti Mkuu wa masuala ya uchumi na maendeleo ya jamii duniani kutoka Taasisi ya WorldFish, Dk Rahma Adam amesema Tanzania ina rasilimali kubwa za bahari, maziwa na mabwawa ambazo zikitumika ipasavyo zinaweza kuinua uchumi wa nchi na maisha ya wananchi kupitia shughuli za uvuvi.
Hata hivyo, amesema baadhi ya changamoto kama vile mabadiliko ya tabianchi, upungufu wa mitaji, elimu sahihi ya uvuvi na uhifadhi pamoja na kukosa teknolojia za kisasa zinakwamisha ukuaji wa sekta hiyo na kufanya mchango wake katika pato la Taifa kuwa mdogo.
Amesema ili mchango wa sekta hiyo uweze kufikia asilimia 10 katika pato la Taifa ni muhimu kwa wavuvi na wachakataji wa mazao ya bahari kupata elimu ya namna gani wanaweza kuvuna na kuhifadhi mazao ya bahari kisasa, litakalosaidia kuongeza uzalishaji na thamani.
“Wakati maeneo mengine duniani mtu mmoja anakadiriwa kula kilo 20 za samaki kwa mwaka, hapa nchini inakadiriwa kula kilo 8.5 kwa mwaka kiwango hiki ni kidogo na kimekuwa kikwazo katika ukuaji wa soko la samaki,”amesema Dk Rahma.
Ameeleza kuwa pamoja na elimu kuna haja ya kuwekeza katika upatikanaji wa teknolojia za kisasa zitakazosaidia uvunaji na uhifadhi wa mazao ya bahari.
“Teknolojia sasa imekua vipo vifaa vinavyoweza kumsaidia mvuvi kujua ni upande upi wa bahari una samaki wengi na upi umevuliwa samaki wengi ili kuacha nafasi kwa samaki kuzaliana tena.”
“Pia hata mvuvi anapopata changamoto ya dhoruba baharini teknolojia hiyo inaweza kufuatilia na kubaini ni wapi alipo ili aweze kupata msaada wa haraka,”amesema.
Dhana potofu kikwazo wanawake kuingia katika uvuvi
Akichangia katika warsha hiyo, Profesa Donatha Timbuhwa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Ndaki ya Sayansi Asilia na Tumizi amesema kuendelea kuwepo kwa dhana potofu dhidi ya wanawake katika jamii kunachangia kuwepo kwa idadi ndogo ya wanawake kushiriki katika shughuli za uvuvi haswa ule unaohusisha maji marefu.
“Baadhi ya jamii zinawazuia wanawake kushiriki katika uvuvi jambo linawanyima fursa ya kunufaika kiuchumi kupitia kushiriki katika uvuvi,”amesema.
Amesema wao kama taasisi ya elimu wameendelea kutoa elimu kwa jamii ili kuwezesha wanawake, vijana pamoja na watu wenye ulemavu kunufaika.
Naye Lydia Gaspare, Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) amesema warsha hiyo imeweka ajenda ya usawa wa kijinsia, ujumuishaji wa watu wenye ulemavu na makundi maalum (GEDSI) kuwa kiini cha mageuzi ya sekta, badala ya kuyaona masuala hayo kama nyongeza ya pembeni.
Amesisitiza kuwa iwapo mapendekezo hayo yatafanyiwa kazi, sekta ya uvuvi inaweza kuwa moja ya nguzo kuu za uchumi wa bluu (blue economy) nchini na kusaidia kufikia azma ya kuongeza mchango wake katika pato la Taifa hadi kufikia asilimia 10 katika miaka ijayo.