1. WFP yaonya hatari ya baa la njaa nchini Somalia
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP limesema hali ya upatikanaji wa chakula nchini Somalia imefikia hatua mbaya ambapo mamilioni ya watu wako hatarini kukumbwa na njaa kali kutokana na ukosefu wa fedha za msaada.
Taarifaya WFP iliyotolewa leo huko Mogadishu nchini Somalia, imesema wa sasa, watu milioni 4.4 wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, huku karibu milioni moja kati yao wakiteseka kwa njaa kali.
Hali ya ukata ikiendelea, WFP imeonya kuwa huduma zake za dharura za chakula na lishe mjini Mogadishu na maeneo mengine zinaweza kusitishwa ndani ya wiki chache zijazo ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa.
Hatua hii imekuja baada ya nchi hiyo kutangaza hali ya dharura ya ukame kufuatia kukosekana kwa mvua kwa misimu miwili mfululizo, jambo lililosababisha vifo vya mifugo na uharibifu wa mazao.
Ukata wapunguza idadi ya chakula
Ross Smith, ambaye ni Mkurugenzi wa WFP anayehusika na maandalizi ya kukabili dharura, amebainisha kuwa hali inazidi kuwa mbaya kwa kasi ya kutisha na familia nyingi zimepoteza kila kitu.
“Hali inaharibika kwa kasi ya kutisha. Bila msaada wa chakula wa dharura hivi sasa, hali itazidi kuwa mbaya zaidi. Tuko kwenye wakati mgumu; bila hatua za haraka, tunaweza kushindwa kuwafikia watu walio hatarini zaidi kwa wakati, wengi wao wakiwa wanawake na watoto,” amesema.
Mwanamke amemshika mkono mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka miwili katika Kituo cha Afya cha Kabasa kinachofadhiliwa na WFP huko Dolow, Somalia.
Sasa mtu 1 kati ya 7 ndiye anapata mgao wa msaada wa chakula
Kutokana na upungufu mkubwa wa fedha, tayari WFP imelazimika kupunguza idadi ya watu wanaopata msaada kutoka milioni 2.2 mwanzoni mwa mwaka 2025 hadi kufikia watu 600,000 pekee.
Hii inamaanisha kuwa kwa sasa shirika hilo linamsaidia mtu mmoja tu kati ya kila watu saba wenye uhitaji mkubwa wa chakula.
Vilevile, mipango ya lishe kwa ajili ya wanawake wajawazito na wanaonyonyesha imepunguzwa kwa kiasi kikubwa, jambo ambalo limeongeza hofu ya kuongezeka kwa utapiamlo kwa watoto wadogo nchini humo.
Ross Smith amekumbushia mafanikio ya mwaka 2022 ambapo njaa kama hii iliepukwa kupitia msaada wa kimataifa, akisisitiza kuwa shirika linao uwezo wa kutoa huduma iwapo rasilimali zitapatikana.
“Mwaka 2022, WFP ilidhihirisha kuwa tukiwa na rasilimali, tunaweza kuongeza juhudi na kuwafikia watu wakati wanapotuhitaji zaidi. Ikiwa huu msaada wetu mdogo uliobaki utasimama, madhara ya kibinadamu, kiusalama, na kiuchumi yatakuwa makubwa,” ameongeza.
Dola milioni 95 zahitajika
Shirika hilo linahitaji kiasi cha dola milioni 95 za Marekani ili kuendelea kusaidia watu wenye uhitaji kuanzia mwezi Machi hadi Agosti mwaka huu.
Misaada ya kibinadamu nchini Somalia ipo kwenye hatua za lala salama ambapo hatua za haraka za Jumuiya ya Kimataifa zinahitajika. Ikiwa fedha hazitapatikana, WFP italazimika kusitisha kabisa misaada yote ya kibinadamu ifikapo mwezi Aprili mwaka huu.
Walinda amani wa UNMISS wakitembelea nyumba ya watoto yatima huko Juba, Sudan Kusini.
2. Matumaini katikati ya migogoro: Kituo cha watoto yatima cha Juba chawapa watoto fursa ya pili
Sudan Kusini ambako mizozo inaendelea kuvuruga utoto wa watoto, kituo kidogo cha watoto yatima katika mji Mkuu Juba kinawapa makumi ya watoto walio hatarini si tu makazi, bali pia matumaini, uponyaji, na nafasi ya kujenga upya mustakabali wao. Anold Kayanda na taarifa zaidi.
Katika Sudan Kusini, watoto wako mstari wa mbele wa migogoro, wakipoteza maisha yao, kutekwa nyara au kupewa majukumu kwa nguvu katika makundi ya kijeshi, pia kunyimwa fursa ya elimu pamoja na huduma muhimu za afya. Wengi pia hupoteza wanafamilia wao, wakiwemo wazazi, na hukabiliwa na kutelekezwa kimwili na kihisia.
Katika kituo cha watoto yatima cha Confident Children out of Conflict (CCC) kilichopo Juba, watoto 52 walioathiriwa zaidi wamepata mahali salama pa kukimbilia. Kibende Anna ni mmoja wao
“Nilipelekwa kwenye eneo hili. Nikaishi hapa. Walinitunza vizuri. Walinipatia vitu vingi kama nguo. Walinipa chakula na maji. Niliishi nikiwa na afya. Na nilipokua kidogo, nikiwa na miaka mitano, nilisajiliwa shuleni. Ninasoma na kujifunza vitu vipya, hata Kiingereza. Ndiyo, na kuandika.”
Sasa akiwa na umri wa miaka 19, Kidende ni mmoja wa watoto wakubwa wanaojitolea muda wao kujenga maisha bora kwa ajili yake na wale wanaomzunguka. Anawahudumia wadogo kwa kuwapatia msaada wa kimwili na kihisia. Kipaumbele chake ni kuhakikisha wanapata fursa ya kufikia uwezo wao kamili maishani licha ya changamoto walizopitia.
“Wengi wao walikuja na kunikuta hapa. Kwa kuwa walikuwa wapya, walikaa kimya. Hawakuwa na imani kwa sababu hawakutujua kwa majina na hawakuweza kutuita. Lakini baada ya muda kupita, kama miezi au siku, basi tunajuana majina. Tunacheza pamoja; tunataniana wakati mwingine. Mara nyingi, wakati mwingine pia tunagombana na kupigana, lakini tunashauriana na kusameheana. Tunaishi maisha rahisi tu hivyo.”
Marion Palm-Eggert, Mshauri wa Polisi katika Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) ambao walikusanyika pamoja kusaidia watoto katika kituo cha watoto yatima cha Sudan Kusini huko Juba.
Kituo hiki cha watoto yatima kilianzishwa mwaka 2007 kinachoendeshwa kwa kiasi kikubwa na walezi wa kujitolea kinalenga kuwajengea wakazi na watoto wapya wanaowasili maadili imara ambayo yameibadilisha taasisi hii kuwa familia.
Bida Samson Robert ni meneja wa kituo anaeleza furaha yake.
“Ninafurahi kwamba watoto wote wanapendana kama kaka na dada. Hili ni jambo tulilokwisha kupanda katika fikra zao ili kuwalea kwa ajili ya baadaye. Wanaweza kutoa mawazo kwamba nataka kuwa hivi au vile. Katika maisha yao ya awali ilikuwa vigumu sana, lakini sasa wanaweza kufunguka na kusema, ‘Samson, nataka kuwa…’”
Kituo hiki kinasaidiwa na wadau wengi wa ndani na kimataifa pamoja na walinda amani wanaohudumu katika Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Sudan Kusini, (UNMISS), ambao hutumia muda wao wa ziada na kuchangia rasilimali zao binafsi ili kuendeleza shughuli za makazi hayo ya watoto na kudumisha maono yake ya mustakabali bora. Marion Palm‑Eggert, ni Mshauri wa Polisi katika UNMISS anasema, “tuliweza kulipia ada za shule kwa mwaka ujao kwa watoto. Hivyo, mwaka mmoja zaidi salama wa elimu. Na tunajua elimu ni ufunguo. Kwa hiyo ndiyo, inanigusa sana.”
Kuwapatia watoto uwezo wa kuunda mustakabali wao wenyewe hakuwanufaishi wao binafsi tu, bali pia kuna athari chanya kwa jamii kwa ujumla, kwa kuweka mfano kwamba mtu yeyote anaweza kufanikiwa kwa motisha sahihi na msaada mdogo tu.
WHO yaunga mkono kampeni ya dharura ya kutoa chanjo nchini Malawi baada ya kubainika kwa mgonjwa wa polio.
3. WHO yaunga mkono kampeni ya dharura ya kutoa chanjo nchini Malawi baada ya kubainika kwa mgonjwa wa polio
- Mgonjwa ni mtoto wa miaka saba ambaye hakuwahi kupata chanjo ya polio.
- Takribani watoto milioni 1.3 wamepatiwa chanjo katika wilaya nane za Kanda ya Kusini
- WHO imeisaidia serikali kuratibu kampeni ya chanjo na kuimarisha ufuatiliaji wa mlipuko.
Takribani watoto milioni 1.3 nchini Malawi wamepatiwa chanjo ya polio katika kampeni maalum ya siku nne, kufuatia kugunduliwa kwa mgonjwa mpya wa polio mwishoni mwa mwezi Januari 2026. Huyu ni mgonjwa wa kwanza kuripotiwa tangu mwaka 2022, wakati virusi vya polio pori vilivyokuwa na uhusiano wa kijenetiki na mlipuko ulioripotiwa nchini Pakistan vilipobainika.
Kampeni hiyo maalum ilitekelezwa kwa kutumia chanjo mpya ya matone ya polio aina ya pili, nOPV2, kwa mujibu wa mwongozo wa muongozo wa kutokomeza ugonjwa huo ambao unaopendekeza utoaji wa chanjo za nyongeza mara tu virusi vya polio vinapogunduliwa.
Shirika la Umoja wa Mataifa la afya duniani,WHOlimekuwa na mchango mkubwa kuanzia maandalizi mpaka utekelezaji wa kampeni hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Afya ya Malawi. WHO ilisaidia kuratibu upokeaji na usambazaji wa dozi milioni 1.7 za chanjo zilizowasili tarehe 10 Februari 2026, na kuhakikisha zinasambazwa ndani ya saa 12 katika wilaya nane za Kanda ya Kusini ili zoezi lianze mara moja.
Aidha, WHO ilitoa msaada wa kitaalamu katika upangaji wa operesheni ya chanjo ya dharura, ikaandaa mafunzo kwa wahudumu wa afya, ikawezesha uimarishaji wa mifumo ya ukusanyaji na uchambuzi wa takwimu ili kufuatilia maendeleo kwa wakati halisi, pamoja na kufanya tathmini ya ubora wa kampeni baada ya zoezi kukamilika.
Mfanyakazi wa afya aakimpatia chanjo ya polio mtoto mchanga nchini Malawi.
Takribani asilimia 97 ya watoto waliolengwa walifikikiwa, huku wilaya ya Blantyre ikivuka lengo kwa kufikia asilimia 109. Duru mbili zaidi za kitaifa zimepangwa kufanyika baadaye mwaka huu, pamoja na kuwafikia watoto zaidi ya elfu 42 waliokosa chanjo katika awamu ya kwanza.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo, Naibu Waziri wa Afya na Usafi wa Mazingira wa Malawi, Dkt. Charles Chilambula, amesema polio ni ugonjwa unaoweza kusababisha ulemavu wa kudumu au hata kifo, lakini unaweza kuzuilika kupitia chanjo, usafi binafsi na mazingira safi.
Kwa upande wake, Kaimu Mwakilishi wa WHO nchini Malawi, Dkt. Charles Njuguna, amesema, “Kampeni hii ni mfano wa juhudi madhubuti na zilizoratibiwa vyema za kukatiza maambukizi ya polio. WHO itaendelea kuisaidia Malawi katika kuhakikisha kila mtoto analindwa dhidi ya ugonjwa huu unaosababisha ulemavu mkubwa lakini unaozuilika kwa chanjo.”
Uchunguzi umebaini kuwa mgonjwa huyo alihusishwa na virusi vya polio vinavyotokana na chanjo aina ya pili vilivyogunduliwa katika mazingira na kwa mtoto wa miaka saba ambaye hakuwahi kupatiwa chanjo. Virusi hivi hujitokeza katika jamii zenye kiwango cha chini cha chanjo na husambaa kupitia maji au chakula kilichochafuliwa.
Mamlaka za afya, kwa msaada wa Umoja wa Mataifa, zinaendelea kufuatilia hali hiyo kwa karibu ili kuhakikisha hakuna wagonjwa wapya na kwamba kila mtoto analindwa dhidi ya polio.