
Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric akizungumza na waandishi wa Habari jijini New York, Marekani Alhamisi Februari 19 amesema, MONUSCO inafanya hivyo kwa kuzingatia majukumu yake ili hatimaye kuboresha upatikanaji wa haki na kupunguza msongamano magerezani.
Katika jimbo la Ituri, mashariki mwa DRC, MONUSCO inasaidia juhudi za kupunguza msongamano katika gereza la Aru, ambapo msongamano na ucheleweshaji wa muda mrefu kabla ya kusikilizwa kwa kesi umeibua wasiwasi.
“Tangu mwanzo wa wiki hii, MONUSCO imekuwa ikitoa utaalamu wa kiufundi na msaada wa vifaa kwa ajili ya vikao vya mahakama zinazoendesha shughuli zake kwa njia ya simu ndani ya gereza hilo. Mahakama hizo zimetumwa kutoka Mahakama ya Kijeshi ya Gereza la Bunia, mji mkuu wa jimbo hilo,” amesema Dujarric.
Kwa mujibu wa msemaji huyo, mpango huo utawezesha kusikilizwa kwa kesi za zaidi ya wafungwa 100 walioko kizuizini.
Kabla ya kusikilizwa kwa kesi zao, wengi wao wamekuwa wamezuiliwa tangu kutangazwa kwa hali ya hatari jimboni Ituri mwaka 2022.
“Hatua hiyo maalum ya kiusalama ilianzishwa ili kusaidia mamlaka kukabiliana na ghasia za makundi yenye silaha zinazoendelea katika eneo hilo,” amefafanua Dujarric,
Mbali na kuunga mkono uendeshaji wa mahakama za simu, ujumbe wa UN pia unarahisisha uwekaji wa kumbukumbu za mahakama za kijeshi katika mfumo wa kidijitali.
“Hatua hiyo inalenga kuongeza uwazi, kuboresha ufanisi, na kuhakikisha ushughulikiaji wa kesi kwa wakati ndani ya mfumo wa haki wa kijeshi,” amesema Dujarric.
MONUSCO imekuweko DRC tangu mwaka 2010 ukiwa na mamlaka yanayojumuisha ulinzi wa raia na kusaidia kuleta utulivu pamoja na kuimarisha taasisi za serikali.