Dar es Salaam. Baadhi ya wakazi wa Tabata Relini, Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, wamelazimika kuyakimbia makazi yao baada ya mafuriko kufurika na kuzingira nyumba zao kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha.

Mwananchi limefika leo katika eneo hilo na kushuhudia baadhi ya nyumba zikiwa zimezungukwa na maji yanayokaribia kufikia usawa wa madirisha, huku wakazi wake wakiwa tayari wamehama kwa hofu ya usalama wao.

Katika maeneo ya Amani na Aloma, Mtaa wa Tabata Relini, takribani nyumba sita zimeathirika kwa kuzungukwa na maji mengi yaliyoingia hadi ndani ya makazi ya watu.

Akizungumza na Mwananchi, Mjumbe wa mtaa huo, Hashimu Hemedi, amesema mafuriko hayo yamesababishwa na kuziba kwa makaravati ya reli, hali iliyosababisha maji kushindwa kupita katika njia zake za asili na hivyo kufurika kwenye makazi ya wananchi.

Amesema jitihada zinahitajika haraka kufungua makaravati hayo ili kupunguza athari zaidi, huku akiwataka wakazi kuwa waangalifu na kuchukua tahadhari wakati huu wa mvua.

Wananchi wa Tabata relini jijini Dar es Salaam, wakimwonyesha mwandishi wa Mwananchi Communications Ltd, nyumba zilizokumbwa na mafuriko kutokana na mvua iliyonyesha jana. Picha na Michael Matemanga

Ameeleza kuwa hali hiyo imesababisha usumbufu mkubwa kwa wakazi, ambao wamelazimika kuyakimbia makazi yao tangu usiku wa Ijumaa, Februari 20, 2026.

Hemedi amsema wakazi wamepata hasara ya mali mbalimbali zilizoharibiwa na maji, huku baadhi ya majengo yakipasuka na kuta kubomoka kutokana na nguvu ya maji.

Kuhusu msaada walioupata, wakazi hao wamesema Jeshi la Zimamoto na Uokoaji lilifika eneo hilo usiku wa tukio kwa ajili ya kutoa msaada, ingawa hadi sasa hali bado haijarejea kuwa ya kawaida.

Wakizungumzia hatua wanazotarajia kuchukuliwa, wameiomba Serikali kuingilia kati kwa haraka ili kuzibua makaravati ya reli yaliyosababisha maji kushindwa kupita katika njia zake, hatua ambayo wanaamini itasaidia kupunguza na hatimaye kuondoa mafuriko hayo.

Wamesema  karavati hizo zimekuwa zikisababisha mara kadhaa kadhia hii hivyo na walisshawasilisha malalamiko yao kwa Sherika la reli (TRC), ambalo liliwaahidi kufanyia kazi mahitaji hayo.

“Tatizo la mafuriko eneo hili limekuwa sugu sana kila mara mvua zikinyesha.

“Tulishaandika barua kwa wahusika wakatuahidi kufanyia kazi lakini mpaka sasa imetokea tena. Sisi tunachoomba ni kuzibuliwa kwa karavati zilizoharibika ili kuondoa tatizo hili,” ameeleza mkazi wa eneo hilo, Jackson Kalikumtima.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *