Dar es Salaam. Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam imeendelea kung’ara baada ya kushinda Tuzo ya Ubora wa Huduma (Service Excellence Award) katika sekta ya afya kwa mwaka wa pili mfululizo, ikitambua mchango wake katika utoaji wa huduma bora na kujali wateja.

Tuzo hiyo imetolewa wiki jana katika hafla iliyoandaliwa na Chartered Institute of Customer Management (CICM), taasisi ya kitaaluma inayotambua mashirika yanayoonyesha viwango vya juu vya ubora wa huduma, ubunifu na uongozi katika uzoefu wa wateja.

Katika kipengele cha sekta ya afya, taasisi sita ziliteuliwa kuwania tuzo hiyo, huku Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam ikiibuka mshindi wa jumla.

Ushindi huo wa mwaka wa pili mfululizo unaakisi uwekezaji endelevu wa hospitali hiyo katika kuimarisha mifumo ya ubora, matumizi ya teknolojia za kidijitali na kuendeleza viwango vya ubora wa huduma za kitabibu.

Mwaka 2025, hospitali hiyo iliunganisha mfumo wa kielektroniki wa kumbukumbu za wagonjwa (MEDITECH Electronic Health Record – EHR) katika mtandao wake wa kitaifa wa huduma za afya, hatua iliyosaidia kuimarisha uratibu wa matibabu na ufanisi wa kiutendaji.

Katika mwaka huohuo, hospitali hiyo ilipokea kwa mara ya nne muhuri wa ubora wa kimataifa (Gold Seal of Approval) kutoka Joint Commission International (JCI), na kuendelea kuwa hospitali pekee nchini Tanzania yenye ithibati hiyo inayotambulika kimataifa.

Aidha, huduma za maabara za hospitali hiyo zilitambuliwa miongoni mwa Maabara 10 bora barani Afrika kwa utendaji wa kipimo cha Immunoassay na Randox International Quality Assessment Scheme (RIQAS).

Taasisi hiyo pia ilitunukiwa Tuzo ya Bingwa wa Mapambano dhidi ya Usugu wa Vimelea kwa Dawa (AMR Champion Award) katika Mkutano wa Saba wa Kisayansi wa Wiki ya Uhamasishaji wa Usugu wa Vimelea Barani Afrika.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo kwa niaba ya hospitali, Meneja wa Rasilimali Watu, John Msangi, ameeleza shukrani na fahari kwa mafanikio hayo, akisema yametokana na juhudi za pamoja za wafanyakazi na uongozi wa taasisi hiyo.

“Tuzo hii ni uthibitisho wa dhamira yetu ya kuweka mgonjwa katikati ya huduma zetu na kuendelea kuboresha uzoefu wa wagonjwa kwa viwango vya kimataifa,” amesema.

Kwa tuzo hiyo ya karibuni, Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam imeimarisha nafasi yake kama kinara wa ubora wa huduma katika sekta ya afya nchini, huku ikiweka viwango vipya vya utoaji huduma bora kwa manufaa ya wananchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *