
Arusha. Mkutano wa dharura wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) unatarajiwa kufanyika Machi 7, 2026 kujadili njia mbadala ya nchi wanachama kuchangia uendeshaji wa jumuiya hiyo ili kutekeleza wajibu wa kisheria wa kutoa michango kwa wakati ili kuiwezesha kutekeleza wajibu wake.
Rais wa Kenya, Dk William Ruto ambaye ni Mwenyekiti wa wakuu wa nchi za EAC ameitisha mkutano huo unaotarajiwa kufanyika jijini Arusha yalipo makao makuu ya jumuiya hiyo iliyoasisiwa mwaka 1999 na marais watatu, Rais Ali Hassan Mwinyi wa Tanzania, Rais Daniel Arap Moi wa Kenya na Rais Yoweri Museveni wa Uganda.
Nchi za Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda kwa muda mrefu zimekua zikitimiza wajibu wao ulioanishwa kikanuni kwa kila nchi mwanachama kuchangia kila mwaka, lakini baadhi ya nchi zimekua nyuma kutimiza wajibu huo ambao umegeuka kuwa mzigo kwa nchi zinazotimiza wajibu wake.
Baraza la Mawaziri wa EAC lilipendekeza njia mbadala ambayo nchi wanachama kuchangia kulingana na kiwango cha uchumi wake (GDP) kama zinavyochangia michango yake kwenye Umoja wa Afrika (AU) jambo ambalo lingeifanya nchi ya Kenya kutoa fedha zaidi ya nchi nyingine hatua iliyopingwa na Kenya.
Hadi Januari 31, 2026 nchi mbili za Tanzania na Kenya zilikua zimechangia kwa asilimia 100, huku nchi nyingine zikiwa zimetoa kwa viwango tofauti hatua inayokwamisha shughuli za jumuiya hiyo zikiwemo wafanyakazi kutokulipwa mishahara kwa wakati, na kulipwa nusu ya posho ya kujikimu wanapokua safari za kikazi .
Inaelezwa zaidi ya dola za Marekani 89 milioni hazijawasilishwa katika Sekretariati ya EAC hatua inayokwamisha shughuli za mihimili ya jumuiya hiyo ambayo ni Sekretariati, Bunge la EALA na Mahakama ya EACJ.
Mkutano huo pia utakuja na mapendekezo madhubuti ya namna ya uendeshaji wa jumuiya hiyo kupitia mpango mpya wa uchangiaji tofauti wa sasa ambao kila nchi inapaswa kuchangia dola za Marekani milioni saba ambazo utumika kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za mihimili mitatu ya EAC pamoja na taasisi zake.
Pia, mpango wa kupunguza matumizi ya jumuiya unalenga kuifanya taasisi hiyo kuwa ndogo yenye tija kubwa kwa wana jumuiya ya Afrika Mashariki ikitajwa kuwa na wafanyakazi 400.
Nafasi ya Katibu Mkuu wa EAC
Tangu kuanzishwa kwa EAC mwaka 1999 nafasi ya juu ya jumuiya hiyo ya Katibu Mkuu imekua ni kupokezana kutoka nchi moja hadi nyingine hatua ambayo ililenga kuimarisha umoja na mshikamano ili kufikia malengo makuu ya kuanzishwa kwake.
Makatibu wakuu waliowahi kushika wadhifa huo ni Francis Muthaura (Kenya), Amanya Mushega (Uganda), Balozi Juma Mwapachu (Tanzania), Dk Richard Sezibera (Rwanda), Balozi Liberat Mfumukeko (Burundi), Dk Peter Mathuki na Veronica Nduva kutoka nchi ya Kenya ambao awamu ya Kenya inakoma mwezi Machi mwaka huu.
Katika mkutano huo wa wakuu wa nchi za EAC unatarajiwa kuja na jina la Katibu Mkuu mpya atakayeongoza taasisi hiyo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo huku nchi za Tanzania, Uganda na Sudani Kusini zikitajwa kutoa Katibu Mkuu mpya.
Nchi za Tanzania na Uganda zinapewa nafasi kubwa kutokana na kuwa ni waanzilishi wa jumuiya na wamekua wakichangia michango kwa wakati hatua inayoweza kupewa kipaumbele wakati wa vikao vya Wakuu wa nchi wanachama mwezi ujao.
Mhadhiri Mwandamizi wa Sheria za Kimataiafa wa Chuo Kikuu cha Makumira (Tuma), Profesa Elifuraha Laltaika amesema kuwa ni bahati mbaya sana kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kutochangia fedha za kuendesha jumuiya hiyo kwa wakati kuwa dalili ya kutokua na utashi wa kisiasa.
“Pamoja na kuwa Rais wa Kenya, Dk William Ruto kuitisha mkutano wa dharura ni jambo zuri, lakini ajenda ya nchi kutochangia jumuiya isingetakiwa kuwepo kabisa,hii jumuiya ni mfano wa jumuiya zingine barani Afrika.
“Pia, ni dalili kwamba jumuiya ina safari ndefu ya kuwa People Centered (Jumuiya iliyojikita kwa wananchi) kwa inavyoonekana, bado ipo katika ngazi ya viongozi zaidi ndiyo maana kiongozi asiyeona umuhimu anaweza kuchelewesha au kutolipa michango,” amesema Profesa Laltaika.
Ameongeza kuwa michango ya kila nchi mwanachama ndiyo uhai wa uendeshaji wa jumuiya hiyo na kusikitishwa na mtazamo wan chi waanzilishi kuweka mbele wazo la kupanua masoko ya bidhaa zao bila kuzingatia uwezo na utashi wa kisiasa kuchangia jumuiya.
Profesa Laltaika amesema nchi kutokuchangia michango ya kisheria ya kila mwaka ni hatua moja nyuma ya kutokuunga mkono mtangamano wa kikanda kwasababu shughuli za EAC zinategemea fedha za nchi wanachama.
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) inaundwa na nchi nane ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudani Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Somalia.