
Arusha. Wakati Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba akitarajiwa kuanza zira ya siku tatu mkoani Arusha, kuanzia kesho baadhi ya wananchi wa mkoa huo wameeleza wanayoyatarajia katika ziara hiyo.
Dk Mwigulu anatarajiwa kuanza ziara kuanzia kesho Februari 22, 2026 hadi Februari 24 katika wilaya tatu za mkoa wa Arusha, baadhi ya wananchi hao wameeleza kuwa wanatarajia ziara hiyo itatatua changamoto mbalimbali ikiwemo migogoro ya ardhi, changamoto ya miudnombinu ya barabara pamoja na upatikanaji wa maji.
Wameeleza kuwa wanaamini kupitia ziara hiyo kama ambavyo ameweza kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika maeneo mengine, pia mkoani Arusha changamoto zoa zitatatuliwa ikiwa ni pamoja na migogoro ya muda mrefu.
Wakizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Februari 21, 2026 baadhi yao wameeleza kumekuwa na changamoto kubwa za migogoro ya ardhi na miundombinu mibovu ya barabara hali inayochangia kuathiri shughuli za kijamii na kiuchumi.
Mmoja wa wananchi hao kutoka Kata ya Muriet, Elias Jonathan, amesema kuwa kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama wakati wote hali inayowafanya kutumia muda mrefu kwenda kutafuta maji.
“Kiukweli sisi wakati mwingine tunateseka maji yanakatika bila kupata taarifa hali inayotulazimu kutumia muda mrefu kwenda kutafuta maji, licha ya kuwa tunasikia miradi mikubwa ya maji lakini kumekuwa na changamoto ya maji wakati mwingine bila taarifa,” amesema.
Naye Naiman Laizer, amesema katika Jiji la Arusha baadhi ya barabara ikiwemo barabara za ndani zimekuwa katika hali mbaya hali inayosababisha msongamano wa magari wakati mwingine pamoja na kuathiri shughuli za kiuchumi.
“Kiukweli barabara nyingi za ndani ni mbovu, tumepiga kelele sana na tunaamini kupitia ujio wake akiwa kama Mtendaji Mkuu wa Serikali, atatusaidia kutatua kero hii ambayo tunaamini kwa mamlaka yake tutapata majibu na barabara zitatengenezwa.”
Mkazi mwingine wa mkoa huo, Neema Wilfred, amesema migogoro ya ardhi bado ni changamoto kubwa katika mkoa huo hasa katika maeneo ya pembezoni.
“Wengine kwa kutokujua sheria na taratibu wanadhulumiwa ardhi, nyumba au mashamba na kwa kukosa uelewa wengine masuala yao yamefikishwa katika ofisi mbalimbali lakini hazijatekelezwa. Tunatamani akiwa anasikiliza kero hizo,tupate ufumbuzi.
“Kumekuwa na migogoro mingi hadi mingine ya wilaya na wilaya au vijiji na vijiji, tunaamini kwa ujio wake migogoro mingi itatatuliwa, wananchi wanyonge wasiojua pa kukimbilia watapata haki zao,” ameongeza.
RC azungumzia ujio huo
Akizungumzia ujio wa Waziri Mkuu, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla amesema kiongozi huyo atafanya ziara ya kikazi kwa siku tatu katika wilaya za Arusha, Arumeru na Longido.
Amesema katika ziara hiyo, Waziri Mkuu atatembelea, kukagua na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali pamoja na kufanya mikutano ya hadhara ambapo wananchi watasikilizwa kero zao mbalimbali.
Amesema atatembelea na kukagua miradi mbalimbali ambapo kesho ataanzia katika wilaya ya Arumeru atakapoweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa bweni la kisasa la Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela (NM- AIST), upanuzi hospitali ya Wilaya ya Oturmet na kufanya mkutano wa hadhara Ngaramtoni.
Amesema Februari 23, 2026 kiongozi huyo atakuwa wilayani Longido ambapo atapokea taarifa ya mradi mkubwa wa maji katika Kata ya Sinya, atazindua mradi wa Shule ya Sekondari Sinya, kutembelea Kituo cha utoaji wa huduma za Pamoja (One stop Border Post), Namanga na kumalizia kwa mkutano wa hadhara wa wananchi Namanga.
Mkuu huyo amesema Februari 24, 2026 atahitimisha ziara hiyo Wilaya ya Arusha ambapo atakagua maendeleo ya ujenzi wa kituo Kikuu cha mabasi Jiji la Arusha eneo la Bondeni City, kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa soko la Kilombero pamoja na mkutano wa hadhara sokoni hapo.
“Baada ya kumaliza siku hizo tatu, ataenda Dodoma kwenye majukumu mengine ya kichama, atarejea kuendelea na ziara katika wilaya zingine tatu ambazo ni Monduli, Karatu na Ngorongoro. Niwaombe wananchi mjitokeze kwa wingi katika mikutano hiyo ambapo atasikiliza kero mbalimbali.”