Arusha. Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Geita imetupilia mbali ombi la Daniel James, aliyekuwa akiomba kuongezewa muda wa kisheria ili aweze kuwasilisha maombi ya mapitio ya mahakama kupinga uamuzi wa kusitishwa ajira yake katika utumishi wa umma.

Maombi hayo namba 32222/2025, yaliwasilishwa dhidi ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Walimu Tanzania (TSC), Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe.

Mwombaji huyo aliwasilisha maombi ya ruhusa ya kuomba mapitio ya Mahakama dhidi ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais ambaye alithibitisha kusitishwa ajira yake katika utumishi wa umma, Agosti 6, 2023.

Uamuzi huo umetolewa Februari 20, 2206 na Jaji Griffin Mwakapeje aliyekuwa akisikiliza maombi hayo.

Jaji Mwakapeje amesema baada ya kuzingatia kwa makini hoja za pande zote, Mahakama imebaini kwamba suala pekee la kuamuliwa ni kama mwombaji ameonyesha sababu ya kutosha ya kuhalalisha kuongezewa muda.

Amesema ruhusa ya kuleta mapitio ya Mahakama ilipaswa kuwasilishwa ndani ya miezi sita (hadi Februari 6, 2024) awe amewasilisha, ila rekodi inaonyesha mwombaji hakuchukua hatua hiyo ndani ya muda uliowekwa na badala yake aliwasiliana na mahakama miezi 11 baada ya muda wa kisheria kuisha bila kutoa maelezo yoyote.

Amesema ingawa mwombaji alieleza ugonjwa kama sababu ya kuchelewa, lakini ushahidi unaonyesha ugonjwa ulitokea kati ya Februari 2025 hadi Julai 2025, hivyo ugonjwa hauwezi kuwa sababu ya kueleza ucheleweshwaji uliotokea kati ya Februati 2024 hadi Januari 2025.

Katika kiapo chake, James alidai kuwa baada ya kupokea uamuzi huo na kuwasilisha kesi ya madai namba 531/2025 ambayo ilifutwa Februari 24, 2025 kutokana na kuwa na dosari za kisheria.

Alieleza kuwa wakati alipokuwa akijiandaa kurekebisha dosari hizo, aliugua shinikizo la juu la damu kuanzia Februari 28 na kupata matatizo makubwa ya kiafya yaliyomfanya asiweze kuendelea na kesi ambapo alilazwa kuanzia Machi 2, 2025 hadi Machi 16, 2025 akipatiwa matibabu.

Alidai kuwa ugonjwa huo ulikuwa nje ya uwezo wake na uliathiri uwezo wake wa kuwasilisha maombi ndani ya muda unaotakiwa na sheria kwa mashauri ya mapitio ya mahakama.

Kwa upande wao, wajibu maombi, walipinga ombi hilo wakidai kuwa mwombaji alishindwa kueleza kipindi chote cha kuchelewa huko na hakuonyesha sababu za kutosha, wakidai kuchelewa huko kulitokana na uzembe wake mwenyewe na kutokuwa makini.

Serikali ilisisitiza kuwa kwa mujibu wa sheria, maombi ya ruhusa ya mapitio ya mahakama yanapaswa kuwasilishwa ndani ya miezi sita tangu tarehe ya uamuzi unaolalamikiwa na kuwa katika maombi hayo muda uliisha Februari 6, 2024.

Alidai kuwa ingawa nyongeza ya muda wa hiari, mwombaji lazima aonyeshe sababu za kutoka kama zinavyohitajika kwa mujibu wa sheria na kudai kuwa utegemezi wake kwa ugonjwa haukutibitishwa kwani ripoti ya matibabu kutoka Hospitali ya Wilaya ya Bukombe.

Ameeleza kuwa ameeleza kuwa aliugua shinikizo la damu lakini hakukuwa na ushahidi wowote unaoonyesha tarehe alizotibiwa na kuhitimisha kuwa kuchelewa kwa maombi hayo kulipita kiasi, hakuna sababu ya kutosha na kuomba yatupiliwe mbali kwa gharama.

Katika maombi hayo, mwombaji huyo hakuwa na uwakilishi wa wakili alisisitiza mahakama kuwa katika kipindi anaugua alishughulikia afya yake badala ya kesi hiyo ya madai na kuiomba Mahakama izingatie hali yake na kukubali ombi hilo.

Uamuzi wa Mahakama

Katika hukumu yake, Mahakama ilikiri kuwa ugonjwa unaweza kuwa sababu ya msingi ya kuongezewa muda pale unapothibitishwa ipasavyo.

Hata hivyo, ilibainisha kuwa ugonjwa wa mwombaji ulitokea baada ya muda wa kisheria kuwa tayari umepita kwa karibu mwaka mmoja, hivyo alipaswa kueleza sababu za msingi zinazokubalika kisheria hasa kabla ya kuugua.

Mahakama ilisema kuwa mwombaji alipaswa kueleza kwa kina kipindi chote cha ucheleweshaji kuanzia Februari 6, 2024 hadi Januari 8, 2025, jambo ambalo hakulifanya.

“Sababu ya kutosha lazima ieleze kipindi chote cha kuchelewa,” ilisema sehemu ya hukumu hiyo, ikiongeza kuwa hata kucheleweshwa kwa siku moja kunapaswa kuelezewa kikamilifu kwa mujibu wa misingi ya kisheria iliyowekwa na mahakama za juu.

Kutokana na hali hiyo, Mahakama ilitupilia mbali ombi hilo kwa kukosa msingi wa kisheria, bila kutoa amri yoyote kuhusu gharama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *