Mbeya. Zaidi ya Sh2.2 bilioni zimetolewa katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya vijijini kwa ajili ya mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi 76  vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Fedha hizo ni sehemu ya makusanyo ya mapato ya ndani ya halmashauri ambazo zimetolewa kwa kipindi cha mwaka 2024/2025 mpaka 2025/2026.

Mratibu wa mikopo ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Consolatha  Kyando amesema leo Jumamosi Februari 21,2026 wakati wa kukabidhi hundi ya mkopo wenye thamani ya Sh 242.9 milioni kwa vikundi 55, vikiwepo vya wanawake 30.

“Kati ya Sh2.2 bilioni Sh959 milioni,  zimenufaisha  vikundi 37 vya wanawake, huku Sh1.2 bilioni, vikundi 36 vya vijana na  Sh27.2 milioni vikundi vitatu vya watu wenye ulemavu ikiwa ni  kutekeleza maelekezo ya Serikali kuwezesha makundi hayo kiuchumi,” amesema.

Kyando amesema miongoni mwa wanufaika wa mikopo hiyo wametoka kwenye Kata za Tembela, Ilungu, Igoma, Itewe, Ijombe, Maendeleo, Ilembo na Santilya.

Nyingine ni Iyunga Mapinduzi, Igale, Bonde la Songwe, Utengule Usongwe, Nsalala, Mshewe, Ikukwa, Ihango, Lwanjilo, Izyra, Masoko, Iwindi, Isuto, Mjele na Itawa.

Amesema mbali na halmashauri kutenga asilimia 10 za mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na walemavu,  bado kuna  changamoto ya baadhi ya vikundi  kutozingatia kanuni, sheria na miongozo ya urejeshaji kwa wakati ili wengine kunufaika.

“Mbali na  changamoto hiyo, lakini vipo baadhi ya vikundi kukosa  miradi yenye tija jambo ambalo limesababisha  kukosa vigezo vya  kunufaika na mikopo ya asilimia 10,” amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Mbeya Agness Elikunda,  amesema  wataendelea kutekeleza malengo ya Serikali kuwezesha wananchi kiuchumi kupitia mikopo ya wanawake, vijana na walemavu.

“Tumekuwa tukitekeleza malengo ya Serikali kuinua kipato cha mtu mmoja mmoja au vikundi vya kijamii kama sehemu ya kutekeleza ilani ya uchaguzi kufikisha huduma muhimu kwa jamii,” amesema.

Kauli ya halmashauri

Upande wake Mwenyekiti Halmashauri, Aida Haule ametaka vikundi vilivyo nufaika na mkopo kutumia kwa malengo yaliyo kusudiwa na kurejesha kwa wakati ili wengine waweze kukopeshwa.

“Fedha hizo zikatumike kwenye miradi ambayo  imejazwa kwenye fomu za maombi na kurejesha kwa wakati kwa kukwepa kutokuwa kikwazo na kujijengea sifa nzuri katika awamu nyingine,” amesema.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Mbeya, Ackim Mwalupindi, amesema mikopo inayotolewa kwa wananchi inazingatia utaratibu wa kisheria, uchambuzi makini na uteuzi wa vikundi vinavyokidhi vigezo bila upendeleo.

“Mikopo hii ni kama mashindano ya mbio; ukianguka leo, jipange kwa awamu nyingine. Kwa walio kosa, wasikate tamaa, wajiandae kwa fursa ijayo,” amesema Mwalupindi.

Hata hivyo, baadhi ya wanufaika wamesema hatua ya Serikali kutoa mikopo kwa asilimia 10 imewapa faraja, hususan kwa wanawake waliokuwa wakiwajibika kimaisha kupitia ndoa.

Sekela Mwakilasa alisema: “Kimsingi Serikali imetufuta machozi ya wake, miaka ya nyuma hali ilikuwa mbaya kutokana na utegemezi katika ndoa, jambo lililosababisha kunyanyasika.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *