
Dar es Salaam. Mtu anapotafuta ajira huweka matumaini makubwa ya kupata kipato cha kuendesha familia, kulipa kodi na kusomesha watoto.
Hata hivyo, matumaini hayo yanaweza kufifia pale mfanyakazi anapokaa miezi kadhaa bila kulipwa mshahara, licha ya kuendelea kutekeleza majukumu yake.
Hayo ndiyo yaliyowakumba wafanyakazi watatu wa kampuni moja ya uendeshaji shughuli za kibiashara jijini Dar es Salaam, waliotumikia kwa miaka kadhaa kabla ya kuachishwa kazi kwa madai ya kudorora kwa biashara.
Baada ya juhudi zao za kufuatilia stahiki zao kugonga mwamba, Februari 19, 2026 waliwasilisha malalamiko yao katika Kliniki ya Sheria Mnazi Mmoja kwa ajili ya kupata msaada wa kisheria.
Akizungumza Februari 20, 2026 kwa niaba ya wenzake, Tresphory Conorage aliyefanya kazi kwa miaka mitatu, amesema waliitumikia kampuni hiyo kwa uaminifu mkubwa hadi walipoambiwa wasitishe kazi kwa sababu biashara imesimama.
“Tulifanya kazi kwa moyo mmoja. Mwenzangu alitumikia miaka nane, mwingine saba na mimi mitatu. Ghafla tukaambiwa tusitishe kazi, huku tukiahidiwa kwamba kukipatikana nafuu tutalipwa haki zetu,” amesema.
Kwa mujibu wa maelezo yao, Nita na Satish wanadai mishahara ya miezi saba kila mmoja, huku Tresphory akidai mshahara wa mwezi mmoja na wiki mbili pamoja na malipo ya likizo na kiinua mgongo.
Kwa jumla, Nita anadai Sh6.2 milioni, Satish Sh9.8 milioni na Tresphory Sh1.46 milioni, fedha zinazozidi Sh17 milioni.
“Tulikuwa waaminifu kazini. Hata tukitumwa kuchukua mizigo ya mamilioni tulifanya bila wasiwasi. Leo hii hatuna hata shilingi,” amesema.
Makubaliano ya malipo kwa awamu
Kupitia usuluhishi wa Kliniki ya Sheria, pande zote zilikutana na kufanya mazungumzo.
Waajiri walikiri kutokuwa na uwezo wa kulipa fedha zote kwa mkupuo, lakini walikubali kulipa kwa awamu nne kuanzia siku 14 baada ya makubaliano yaliyosainiwa Februari 20, 2026.
“Tumeelekezwa vizuri na makubaliano yamefikiwa. Ndani ya siku 14 malipo ya kwanza yataanza kutoka. Kwa upande wangu, nitaingiziwa Sh750,000 leo kutokana na dharura niliyoeleza,” amesema Tresphory.
Wafanyakazi hao wamesema hawakuwa na nia ya kulipiza kisasi bali kupata haki yao halali.
“Sisi ni Watanzania, tumefundishwa kufanya kazi kwa uaminifu. Pesa zitabaki, lakini haki ni muhimu,” wamesema.
Mashauri 25 yapokewa
Akizungumzia mwenendo wa mashauri ya ajira, Wakili wa Serikali Mwandamizi kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Silinde Gumada, amesema tangu kuanza kwa kliniki hiyo Februari 16 hadi Februari 19, 2026, mashauri 25 ya ajira yalikuwa yamepokelewa.
Amesema mashauri hayo yanahusu usimamishwaji wa kazi bila mafao, kuajiriwa bila malipo na kusimamishwa kazi kinyume na mikataba.
“Baadhi ya wafanyakazi wanasema walisimamishwa kazi ghafla bila kupewa barua rasmi wala kulipwa mafao yao ya mwisho.
“Wengi hawajui haki zao, hali inayochangia ukiukwaji wa sheria za kazi. Tunawapa elimu na kuwasaidia kupata haki zao kwa kushirikiana na taasisi husika,” amesema Gumada.
Kliniki hiyo imeendelea kuwa kimbilio kwa wakazi wa Dar es Salaam wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za mawakili, huku ikitoa fursa ya kusikiliza na kutatua migogoro kwa njia ya maelewano.