
Dar es Salaam. Taasisi ya kimataifa ya tathmini ya kiuchumi (Moody’s Ratings) imeendelea kuipa Tanzania alama ya uwezo wa kukopa kwa muda mrefu (B1), jambo linaloashiria kuwa uchumi unaendelea kukua lakini imetahadharisha kuwepo kwa changamoto za umasikini, hatari za kisiasa na matumizi ya Serikali.
Katika taarifa yao iliyotolewa Februari 20, 2026, Moody’s inaeleza kuwa alama hiyo inatokana na mchanganyiko wa mambo chanya na hasi katika uchumi wa Tanzania.
Kwa upande mmoja, uchumi unaendelea kukua kwa kasi na kuonyesha uwezo wa kustahimili mishtuko ya kiuchumi, lakini kwa upande mwingine, masuala ya kiutawala na umasikini wa kipato kwa wananchi vinaendelea kuwa changamoto kubwa.
Moody’s inaeleza kuwa Tanzania inaendelea kuhamia katika mfumo wa uchumi unaotegemea zaidi uwekezaji wa sekta binafsi, jambo linaloonekana kusaidia ukuaji wa uchumi kwa muda mrefu.
Hata hivyo, taasisi hiyo imeonya juu ya ongezeko la hatari za kisiasa kufuatia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 uliogubikwa na vurugu. Kwa mujibu wa Moody’s, hali hiyo haikuathiri sana shughuli za kiuchumi kwa muda mrefu, lakini bado kuna hatari ya kutokea kwa misukosuko ya kijamii siku zijazo kutokana na umaskini, ongezeko la watu na ukosefu wa ajira kwa vijana.
Imeelezwa kuwa endapo hali ya kisiasa itadorora tena inaweza kuathiri uwekezaji, mauzo ya nje na mapato ya Serikali, jambo ambalo linaweza kudhoofisha zaidi uwezo wa nchi kukopa.
Ongezeko la deni la Serikali
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa nguvu ya kifedha ya Serikali imepungua kwa kiasi kidogo kutokana na ongezeko la mikopo kwa ajili ya kugharamia miradi ya miundombinu, huduma za kijamii na ulipaji wa madeni ya nyuma.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa hivi sasa, deni la Serikali limefikia karibu asilimia 50 ya Pato la Taifa (GDP), kiwango ambacho Moody’s inaeleza kuwa bado ni himilivu ikilinganishwa na nchi nyingine zenye kiwango sawa cha maendeleo.
Hata hivyo, gharama za riba zimeongezeka na sasa zinatumia takribani asilimia 16 ya mapato ya Serikali, hali inayoashiria kuwa kuna upungufu wa mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo.
Moody’s inaeleza kuwa licha ya hali hiyo, deni linatarajiwa kubaki katika kiwango hicho kutokana na ukuaji wa uchumi na ongezeko la mapato ya ndani.
Imeeleza kuwa juhudi za Serikali za kuongeza mapato zimeanza kuzaa matunda, hasa kupitia maboresho ya usimamizi wa kodi, matumizi ya mifumo ya kidijitali na kuimarika kwa ufuatiliaji wa walipakodi.
Mapato yasiyotokana na misaada yameongezeka kutoka asilimia 13.7 ya pato la Taifa mwaka wa fedha 2020/21 hadi asilimia 15.9 mwaka 2025/26, huku yakitarajiwa kufikia zaidi ya asilimia 17 katika mwaka wa fedha unaoendelea.
Pia, mapato yasiyo ya kodi, ikiwamo gawio kutoka mashirika ya umma, yameongezeka kufuatia maboresho ya uendeshaji wa mashirika hayo.
Hata hivyo, Moody’s imeonya kuwa mahitaji makubwa ya fedha za miradi ya maendeleo na kijamii yataendelea kuweka shinikizo katika bajeti ya Serikali, hasa wakati ambapo misaada na mikopo nafuu inapungua.
Uchumi kukua zaidi
Wakati Tanzania ikitarajia ukuaji wa uchumi kwa zaidi ya asilimia 6 mwaka huu, Moody’s inaeleza kuwa rasilimali za asili pamoja na maboresho ya miundombinu ya nishati na usafiri, yanaweza kusaidia uchumi wa Tanzania kukua zaidi ya kiwango kinachotarajiwa kwa sasa.
Moody’s imeeleza kuwa ukuaji huo unaweza kusaidia kuongeza kipato cha wananchi na kupunguza shinikizo la kijamii kwa muda mrefu.
Hata hivyo, taasisi hiyo inaonya kuwa changamoto za kimuundo, ikiwamo ongezeko kubwa la idadi ya watu vijana na mahitaji makubwa ya huduma za kijamii, zitaendelea kuhitaji matumizi makubwa ya Serikali.
Changamoto fedha za kigeni
Moody’s pia imeeleza kuwa bado kuna hatari za upatikanaji wa fedha za kigeni kutokana na nakisi ya muda mrefu ya urari wa biashara ya nje.
Ingawa deni la nje linaelezwa kuwa himilivu, historia ya vipindi vya uhaba wa fedha za kigeni imeifanya taasisi hiyo kuendelea kuweka tahadhari kuhusu uwezo wa nchi kuhimili mishtuko ya kifedha kutoka nje.