
Dar es Salaam. Imezoeleka katika jamii kwamba wanaume ndiyo huwatelekeza watoto wao kwa mama zao, jambo linalosababishwa na harakati za utafutaji wa fedha sehemu mbalimbali nchini au nje ya nchi.
Hata hivyo, siku hizi hali ni tofauti. Wanaume nao wanatelekezewa watoto na wake zao kwa sababu tofauti, lakini kubwa ikiwa ni ugumu wa maisha au kukosekana kwa maelewano baina yao.
Hilo limemkuta Patrick Ndege (32), mkazi wa Dar es Salaam, ambaye mke wake amemtelekeza na mtoto mdogo. Mke wake huyo aliondoka nyumbani kwao kwa sababu ya ugumu wa maisha, akitaka vitu ambavyo mumewe hakuweza kumpatia.
Mwananchi lilimtafuta mwanamke huyo (jina limehifadhiwa) ili kujua sababu za kutelekeza familia yake. Hata hivyo, mwandishi alipojitambulisha na kueleza shida yake, mwanamke huyo alisema hamwelewi, hivyo akakata simu na hakupokea tena alipopigiwa.
Kama vile wasemavyo wahenga, maji hufuata mkondo. Patrick naye ni mwathirika kama watoto wengine wanaotelekezwa na mmoja wa wazazi wao. Alilelewa na mama yake pekee baada ya baba yake kuwatelekeza akiwa mdogo.
Maisha yake yanaakisi mzunguko wa maumivu unaojirudia kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Katika mazungumzo yake na Mwananchi Februari 20, 2026, Patrick ameeleza kuwa alilelewa na mama pekee baada ya baba yake kumtelekeza akiwa mdogo.
Patrick amesema alikulia Iringa huku akimsikia baba yake ni mtu wa Kigoma. Hata hivyo, hakuwahi kumwona na sasa anaishi Dar es Salaam akiwa hana ndugu baada ya mama yake kufariki dunia na ndugu yake mmoja kupotezana naye kabla ya yeye kuhamia Dar es Salaam kutafuta maisha.
“Nilikulia kwa mama tu, baba sikuwahi kumjua zaidi ya kusikia habari zake. Baada ya mama kufariki, tukapotezana na ndugu yangu na nikaanza maisha ya kujitegemea mapema sana,” amesema kijana huyo.
Amesema walizaliwa wawili, lakini kifo cha mama yao kilibadili kabisa mwelekeo wa maisha yao kwani kila mmoja alianza kupambana kivyake.
Kisa cha mke kukimbia
Patrick amesema alijifunza na kuanza kazi ya kusuka katika saluni za kike Kigamboni, akilipwa Sh2,000 kwa siku kwa ajili ya nauli na kupata chakula kazini hapo. Kwa kipato hicho kidogo, aliendesha maisha yake na baadaye kuanza familia ambayo iliyumba kutokana na kipato kidogo.
“Nilikuwa namhudumia mke wangu kwa kujibana sana hadi akajifungua salama. Nilifanya kila nilichoweza kuhakikisha hapati shida, lakini baada ya mtoto kuzaliwa na kufikisha miezi miwili, hali ilianza kubadilika ndani ya nyumba. Mara aseme anataka sofa, mara anataka friji, mwisho akasema amechoka haya maisha,” amesimulia Patrick.
Amesema maneno hayo yalimuumiza, lakini aliamua kuvumilia kwa sababu ya mtoto wao: “Nilimrudia Mungu sana kutuliza mawazo yangu na nikawa mwanakwaya maarufu pale Msimbazi. Kwa kuwa ni mama wa mwanangu, nilivumilia kwa ajili ya mtoto.”
Baadaye, amesema alipata kazi nyingine kiwandani ambapo alilipwa Sh5,000 kwa siku, lakini hali haikubadilika. Amesema mke wake alimwambia wazi kwamba siku akimpata mtu mwenye pesa ataondoka na asije kumtafuta.
“Oktoba 2025 aliniambia uamuzi wake wa kuondoka, akasema nimepata mwanaume ana kila kitu ninachokitaka, kaa mbali na mimi. Tukatengana rasmi, akahamia sehemu nyingine,” amesimulia.
Patrick amesema aliendelea kumhudumia na kumtumia fedha za mahitaji ya mwanawe, lakini siku alipokwenda kumwona na kumpelekea mahitaji katika kazi yake mpya, alifukuzwa na kukabidhiwa mtoto wake aondoke naye ili asiendelee kufika hapo.
“Akanipa mtoto wangu na kuniambia sitaki kukuona hapa, usije kuniharibia kwa bwana wangu. Baada ya wiki moja akahama nyumba hiyo na mpaka leo sijui alipo, japo nilisikia tu alipata kazi za ndani Masaki,” amesema.
Maisha baada ya mke kukimbia
Baada ya kupewa mtoto, Patrick aliendelea kufanya kazi ya ulinzi Msimbazi Center, akilipwa Sh120,000 kwa mwezi, lakini amesema baadaye aliachishwa kazi kwa kuwa alilazimika kwenda na mtoto kazini, aliyemlaza akiwa lindoni usiku kucha.
Kwa sasa, Patrick anaishi chumba cha kupanga akilipa Sh30,000 kwa mwezi, akisaidiwa na wasamaria wema kwa chakula na kodi ya pango. Anaendelea kutafuta kazi huku akiwa na mtoto wake huyo, akiamini ipo siku mambo yatabadilika na mwanaye atakuwa katika mazingira bora tofauti na aliyopitia yeye.
Historia ya maisha yake
Patrick amesema maumivu ya utoto wake ndiyo yanayompa nguvu ya kupambana leo katika mapito anayopitia. Baada ya mama yake kufariki, aliachwa bila msaada wa mzazi yeyote na kulazimika kufanya kazi ndogondogo jijini Dar es Salaam ili kujikimu.
“Maisha ya kukosa baba yaliniumiza sana na nilijisikia mpweke, lakini yalinifundisha kupambana. Napambana ili mwanangu asipitie maisha niliyopitia mimi nilipotelekezwa na baba yangu,” amesema.