
Tangu mwanzoni mwa mwaka 2026, mashambulizi matano dhidi ya vituo vya matibabu tayari yamerekodiwa katika mzozo wa Sudan, mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) amesema siku ya Jumamosi, Februari 21. Mapigano kati ya jeshi la serikali na wanamgambo wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) kwa karibu miaka mitatu yamevuruga vibaya mfumo wa afya ambao tayari ni dhaifu: zaidi ya theluthi moja ya vituo vya afya nchini humo havifanyi kazi.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
“Katika siku 50 za kwanza za mwaka 2026, mashambulizi matano dhidi ya vituo vya afya yamerekodiwa nchini Sudan, na kusababisha vifo 69 na majeruhi 49,” ameandika Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus kwenye kurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter.
Shambulio la hivi karibuni lililenga Hospitali ya Al-Mazmoum katika Jimbo la Sennar, kusini mashariki mwa nchi, siku ya Jumapili, Februari 15. Wagonjwa watatu waliuawa. Watu saba walijeruhiwa, akiwemo mfanyakazi mmoja, kulingana na afisa huyo wa Umoja wa Mataifa.
Mwanzoni mwa mwezi Februari, zaidi ya watu 30 waliuawa katika mashambulizi matatu dhidi ya vituo vya matibabu huko Kordofan, ambayo imekuwa moja ya vitovu vya mapigano kusini mwa Khartoum.
Tangu kuanza kwa mzozo huo, WHO imethibitisha angalau mashambulizi 206 dhidi ya vituo vya afya. Mashambulizi haya yamesababisha vifo vya takriban watu 2,000 na mamia kadhaa kujeruhiwa.
Karibu miaka mitatu ya vita imegharimu maisha ya makumi ya maelfu ya watu na zaidi ya watu milioni 14 walitoroka makazi yao.
Umoja wa Mataifa unauita mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu duniani, huku visa milioni 4.2 vya utapiamlo mkali vikiweza kurekodiwa mwaka wa 2026.
Hali ni mbaya; Umoja wa Mataifa unaonya kwamba akiba yake ya misaada ya kibinadamu inaweza kupungua ifikapo mwisho wa mwezi Machi.