
TIMU ya TMA FC ya jijini Arusha, iko katika hatua za mwisho za kumuajiri kocha Mzanzibari, Haji Ali Nuhu, ili kukiongoza kikosi hicho cha Championship hadi mwishoni mwa msimu huu, akichukua nafasi iliyoachwa na mtangulizi wake, Habibu Kondo.
Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa TMA, zimeliambia Mwanaspoti, Ali Nuhu, ndiye anayepewa nafasi zaidi ya kuiongoza timu hiyo hadi mwisho wa msimu huu, baada ya kocha huyo aliyeifundisha pia JKU SC kutoka visiwani Zanzibar kuonyesha utayari.
“Mazungumzo hayo ni kweli yapo na yanaendelea vizuri, tumekaa kwa muda mrefu kidogo bila kufanya uamuzi wowote juu ya suala hilo, ila lengo kubwa lilikuwa pia ni kupata kocha mzuri atakayeendana na mahitaji yetu,” kilisema chanzo hicho.
Kondo aliyezifundisha timu za Mtibwa Sugar, Azam, Coastal Union, Majimaji na Mbeya Kwanza, aliondolewa katika benchi la ufundi na kocha msaidizi, Augustino Thomas, kocha wa makipa, Ally Mustapha ‘Barthez’ na kocha wa viungo, Kigi Makasi.
TMA kwa sasa inafundishwa na aliyekuwa mchezaji wa timu hiyo, Omary Matwiko ‘Tico Tico’, ambapo kabla ya mechi ya jana dhidi ya KenGold iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha, kikosi hicho kilikuwa kinashika nafasi ya 11 kwa pointi 18.