
AZAM FC imepata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mashujaa katika mchezo wa juzi, lakini maswali ya wengi ni wapi alipo kiungo fundi Feisal Salum ‘Fei Toto’.
Baada ya mchezo huo, kocha mkuu wa Azam FC, Florent Ibenge, ameweka wazi sababu ya kutomtumia nyota huyo akieleza kuwa alikuwa anahitaji kupumzika kutokana na uchovu wa mechi nyingi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ibenge alisema Feisal hana majeraha bali aliamua kumpunguzia mzigo ili kulinda afya yake na kuhakikisha anabaki kwenye kiwango bora kuelekea mwisho wa msimu.
Kocha huyo alisema dalili za uchovu zilianza kuonekana katika mchezo dhidi ya Fountain Gate ambao Azam ilishinda mabao 2-0, ambapo Fei Toto alicheza dakika 45 pekee kabla ya kutolewa.
“Feisal tumempa mapumziko, hana majeraha. Tuliona kwenye mchezo uliopita alionyesha wazi kuwa mwili ulikuwa umechoka na haikuwa salama kuendelea kumpa dakika nyingi,†alisema Ibenge.
Aliongeza: “Ni mchezaji muhimu kwetu lakini pia ni aina ya wachezaji wanaotaka kucheza kila wakati. Tulilazimika kuchukua uamuzi huo ili kulinda afya yake.
Pamoja na kutokuwepo kwa Fei Toto, Ibenge aliwapongeza wachezaji wake kwa kuonyesha kiwango kizuri na kupata ushindi dhidi ya Mashujaa, ambao umefanikisha kukata tiketi ya kushiriki mashindano ya Kombe la Shirikisho msimu ujao.
Kocha huyo raia wa DR Congo alisema kiungo huyo atarejea kikosini mara baada ya benchi la ufundi kujiridhisha kuwa ameondokana na uchovu na yuko tayari kumalizia mechi zilizobaki za msimu.
Kutokana na rekodi, ukimuuliza mfuatiliaji au shabiki yoyote wa Ligi Kuu Bara nani ni mfungaji bora wa msimu atakujibu Feisal Salum, kiungo wa zamani wa klabu ya Yanga.
Msimu huu Fei Toto amecheza mechi 25 za Ligi Kuu akitumia dakika 1,992 uwanjani. Ameikosa mechi dhidi ya Mashujaa pamoja na mchezo wa ugenini dhidi ya Tanzania Prisons alipokuwa anatumikia adhabu ya kikanuni baada ya kupata kadi nyekundu dhidi ya Pamba Jiji.
Kiungo huyo pia ndiye kinara wa mabao ndani ya Azam akiwa amefunga mabao 14 na kutoa asisti nane, akihusika moja kwa moja kwenye mabao 22 msimu huu.
Azam itakutana na Yanga katika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB, Juni 21,2026, kwenye Uwanja wa CCM Kirumba. Baada ya hapo itakutana tena na Wanajangwani hao Juni 24 Zanzibar ndani ya Amaan Complex.