
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesisitiza dhamira ya nchi yake kulinda haki halali za taifa katika nyanja ya nishati ya nyuklia kwa njia ya diplomasia.
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran ametoa kauli hiyo wakati wa mazungumzo ya simu na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA), Rafael Grossi, yaliyofanyika mwishoni mwa siku ya Jumamosi.
Katika mazungumzo hayo, Araghchi amesisitiza azma ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuendeleza mawasiliano ya kujenga na kutumia diplomasia ili kulinda haki na maslahi halali ya taifa la Iran katika matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia, kwa mujibu wa Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT) na sheria za kimataifa.
Wawili hao pia wamejadili maendeleo ya hivi karibuni kuhusu mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Marekani na Iran, yanayolenga kufikia uelewano wa haki kuhusiana na suala la nyuklia la Tehran.
Mazungumzo hayo ya simu yalifuatia duru mbili za mazungumzo kati ya maafisa wa Iran na Marekani yaliyoratibiwa na Oman tarehe 6 na 17 Februari, baada ya wiki kadhaa za mvutano unaoongezeka.
Vitisho vya mara kwa mara vya kijeshi vya Marekani vimepelekea Iran kuonya kuwa hata risasi moja ikifyatuliwa dhidi ya ardhi yake, itajibiwa kwa hatua kali na pana.
Siku ya Jumatano wiki iliyopita, Araghchi na Grossi walijadili kwa njia ya simu matokeo ya duru ya pili ya mazungumzo ya Iran na Marekani. Aidha, walikutana pia siku ya Jumatatu katika mji wa Geneva, Uswisi, ambako walibadilishana mawazo kuhusu masuala ya kiufundi yanayohusiana na ushirikiano wa Tehran na IAEA.