
Rais wa Marekani, Donald Trump amekosoa mashambulizi ya Israel dhidi ya Lebanon, na kukiri kwamba kuna hitilafu kati yake na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kuhusu suala la Lebanon.
Akizungumza na waandishi wa habari Jumatano kabla ya kuondoka Ufaransa baada ya kuhudhuria mkutano wa kilele wa G7, Trump alisema kwamba “Israel inafanya mambo mabaya nchini Lebanon.”
Akizungumza kuhusu Netanyahu, Trump aliongeza: “Tunahitilafiana kidogo kuhusu Lebanon, na mimi namwambia Bibi (jina la utani la Netanyahu): “kuwa mtulivu zaidi.”
Trump ameendelea kusema, akimhutubu Waziri Mkuu wa Israel: “Sio lazima kuharibu jengo kila mara mwanachama wa Hizbullah anapoingia kwenye jengo hilo” nchini Lebanon.
Amesema kwamba Netanyahu – ambaye anatafutwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kwa mashtaka ya kufanya uhalifu wa kivita huko Gaza – “wakati mwingine anapatwa na hamaki kidogo..”
Vyombo kadhaa vya habari hivi karibuni vimeashiria mzozo kati ya Trump na Netanyahu kuhusu vita ambavyo Marekani na Israel zilianzisha dhidi ya Iran, na baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wamefikia hatua ya kusema kwamba, uhusiano kati ya wawili hao uko katika hali mbaya zaidi, hasa baada ya Washington kutia saini hati ya maelewano ya kukomesha vita na Tehran.
Matamshi yaliyotolewa na Trump siku ya Jumanne pia yameibua hasira huko Israel, baada ya kusema kwamba Israel “haingekuwepo bila Marekani”.