Sekta ya madini nchini Sudan imepata hasara inayokadiriwa kufikia dola bilioni saba kufuatia kuendelea kwa vita vya vya ndani kwa takribani miezi 34. Hayo ni kwa mujibu wa Mamlaka ya Kitaifa ya Madini ya nchi hiyo.

Akizungumza siku ya Jumamosi, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Utafiti wa Jiolojia, Ahmed Haroun al‑Tom, amesema kuwa “hasara za sekta ya madini nchini Sudan kutokana na vita zimefikia takribani dola bilioni 7.”

Ameeleza kuwa sekta za umma na binafsi zimekumbwa na uporaji na hujuma kutokana na mzozo huo, hali iliyosababisha kupotea kabisa au kwa kiasi kikubwa kwa miundombinu muhimu, na kuleta hasara zinazokadiriwa kuanzia mamilioni hadi mabilioni ya dola katika sekta mbalimbali za uchumi.

Al‑Tom amefichua kuwa shughuli za mamlaka hiyo zimepungua kutoka majimbo 18 kabla ya kuzuka kwa vita hadi majimbo sita pekee kwa sasa, jambo lililoathiri moja kwa moja utafiti wa kijiolojia, shughuli za uchunguzi wa rasilimali, pamoja na mapato ya umma.

Amesema kuwa mamlaka hiyo imeanza kuagiza teknolojia za kisasa na mitambo ya hali ya juu ili kuimarisha uwezo wake wa kiufundi, kufuatia kurejea kwa shughuli zake katika mji mkuu Khartoum badala ya Port Sudan.

Taasisi za serikali zilizohamia Port Sudan mashariki mwa nchi baada ya kuzuka kwa vita sasa zimerejea Khartoum kuendelea na majukumu yao, zikiwemo Baraza la Uongozi linaloongozwa na mkuu wa jeshi Jenerali Abdel Fattah al‑Burhan na Baraza la Mawaziri.

Al‑Tom amebainisha kuwa kabla ya vita vya wenywe kwa wenyewe, mamlaka hiyo ilikuwa na teknolojia za kiwango cha juu katika utafiti na uchunguzi wa madini, lakini nyingi kati ya hizo zilipotea kutokana na athari za vita.

Tangu Aprili 2023, Sudan imekumbwa na vita vya ndani kati ya serikali na kundi la wanamgambo wa RSF ambao sasa serikali inawataja kuwa magaidi. Serikali ya Sudan imekuwa ikiishutumu Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kuwa inawaunga mkono waasi hao ambao wanatenda jinai za kuogofya katika maeneo wanayoyashikilia.
 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *