
MSHAMBULIAJI wa Mbeya Kwanza, Boniface Mwanjonde, amesema ameumia baada ya usajili wake wa kujiunga na Fountain Gate ya Ligi Kuu Bara katika dirisha dogo la Januari 2026 kukwama, ingawa amechukulia ni changamoto za kuzidi kumkuza kimaisha.
Nyota huyo aliyechangia mabao 13, katika mechi 14, alizoichezea Mbeya Kwanza, baada ya kufunga tisa na kuasisti manne, alisajiliwa na Fountain Gate, japo uhamisho huo ulikwama mwishoni kutokana na kikosi hicho kufungiwa kusajili wachezaji.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mwanjonde, amesema aliamini ni muda sahihi kwake wa kuonyesha kipaji chake katika mechi za Ligi Kuu Bara, ingawa kwa bahati mbaya haikuwa hivyo, jambo lililomchukua muda mrefu kurudi katika hali yake ya kawaida.
“Kiukweli ni jambo lililoniumiza sana kuona sijafanikiwa kukamilisha uhamisho huo, ila nashukuru watu wangu wa karibu na hata benchi la ufundi walinisihi niendelee kupambana, kwa sababu wakati sahihi ni wa Mwenyezi Mungu,” amesema Mwanjonde.
Mshambuliaji huyo aliyecheza KenGold, Ndanda na Mbeya City chini ya miaka 20, kisha, Chitipa United ya Malawi, amesema baada ya kukwama Fountain, mabosi wa timu hiyo walitaka kumpeleka JKU ya Zanzibar, ingawa aliomba kurudi Mbeya Kwanza.