Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imelaani vikali hatua ya serikali ya Uganda ya kumpokea kamanda wa waasi wa Rapid Support Forces (RSF), Mohamed Hamdan Dagalo (Hemedti), ikielezea hatua hiyo kuwa ni “msaada wa moja kwa moja kwa uhalifu wa mauaji ya kimbari.”

Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imesema katika taarifa rasmi leo Jumapili kwamba mapokezi ya Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, kwa “kiongozi wa wanamgambo waasi,” katika ikulu ya rais huko Entebbe ni hatua isiyo ya kawaida ambayo inapingana na majukumu ya Uganda kuhusu ujirani mwema na inapuuza sheria zinazosimamia uhusiano kati ya nchi wanachama wa mashirika ya kikanda na kimataifa.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa hatua hii “haiheshimu kiwango cha chini cha maadili ya kibinadamu” na haijali ukubwa wa uhalifu na ukatili unaofanywa dhidi ya raia nchini Sudan, ikisisitiza kwamba serikali ya Sudan hairuhusu ardhi yake au ardhi ya nchi ndugu kutumika kwa ajili ya kusaidia vikosi vya waasi dhidi ya utawala halali na unaotambuliwa kimataifa.

Kuhusu yanayojiri uwanjani, Waziri wa Fedha wa Sudan na kiongozi wa Harakati ya Haki na Usawa, Jibril Ibrahim, amepongeza utendaji wa wapiganaji wake katika vita vya mji wa kimkakati wa Al-Tina katika Jimbo la Darfur Kaskazini dhidi ya wapiganaji wa RSF.

Ibrahim amesema kwamba wapiganaji wa Harakati ya Haki na Usawa “wamewapa wanamgambo wa Rapid Support Forces somo ambalo hawatalisahau kamwe,” akisisitiza haja ya “kufuatilia mabaki ya wanamgambo hao na kusafisha kabisa eneo hilo.”

Taarifa hii imetolewa huku vyanzo vya kijeshi vikithibitisha kwamba jeshi la Sudan na washirika wake vimezima shambulio kubwa lililolenga kudhibiti mpaka muhimu na Chad, ambao hutumiwa na mashirika ya misaada ya kibinadamu kuingiza misaada katika maeneo hayo.

Wakati huo huo, gavana wa Darfur, Minni Arko Minawi, ameelezea upinzani wake dhidi ya ziara ya Mohamed Hamdan Dagalo nchini Uganda, akisisitiza kwamba kumpokea “Hemedti” kunatafsiriwa kama “kukubali kimya kimya uhalifu ambao umefikia kiwango cha mauaji ya kimbari.”

Mkutano wa Rais Museveni na Mohamed Hamdan Dagalo huko Entebbe unahesabiwa kuwa ni kudhihiri hadharani kwa mara ya kwanza kwa Hemedti tangu Septemba mwaka jana. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *