MOROGORO: JUMLA ya vijana 42,000 wamenufaika na programu za muda mrefu na muda mfupi kwa kupatiwa elimu na mafunzo ya ufundi stadi kupitia Mradi wa Mpango wa Elimu Changamani kwa Vijana Walio nje ya Shule (IPOSA) unaotekelezwa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW).
Mpango huo unalenga makundi mahsusi ya vijana ambao hawakuwahi kwenda shule, walioacha shule katika ngazi ya msingi, sekondari, waliomaliza darasa la saba na hawakupata fursa ya kuendelea na elimu ya sekondari.
Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Taasisi hiyo, Profesa Philipo Sanga amesema hayo wakati akimkaribisha Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Hussein Mohamed Omar kufungua mkutano wa 16 wa Baraza la Wafanyakazi wa Taasisi hiyo .
Naibu Katibu mkuu huyo, hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Elimu Msingi wa wizara hiyo, Abdul Maulid.

Profesa Sanga ambaye pia ni Mkuu wa Taasisi hiyo amesema kupitia mradi huo vijana 12,000 wamenufaika na programu za muda mrefu ambapo wavulana ni 5,406 na wasichana 6,594 na wengine 30,183 wakinufaika na program ya muda mfupi kwa kupatiwa elimu na mafunzo ya ufundi stadi.
Amesema kupitia mradi huo, Taasisi ilifanikiwa kupata fedha kiasi cha USD 400,000 kwa ajili ya ujenzi wa karakana tatu za mfano.
Profesa Sanga amesema karakana moja imejengwa mkoa wa Manyara na imekamilisha ujenzi kwa asilimia 99 na kazi iliyobaki ni ya kuweka milango na madirisha pekee na nyingine mkoa wa Shinyanga ujenzi umefikia asilimia 70 , wakati Tanga umefikia asilimia 75.

Amesema karakana hizo zitaendelea kuwasaidia vijana walio nje ya mfumo rasmi wa shule kupata ujuzi wa mafunzo ya ufundi, Stadi za Maisha, Ujasiriamali na Stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK).
Katika mradi wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari kwa njia mbadala nchini (SEQUIP-AEP).ulianza kutekelezwa mwaka 2022 kufikia ukomo mwaka huu (2026) alisema hadi 2025, jumla ya wasichana 13,272 walisajiliwa.
Profesa Sanga amesema wasichana hayo ni waliokuwa wamekatiza masomo ya sekondari na kuendelea na masomo na hivyol kuvuka lengo kwa asilimia 111 ya kusajili wasichana 12,000 kulingana na agizo la Serikali hadi kufikia mwaka 2026
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu huyo kwenye hotuba hiyo aliipongeza Taasisi kwa kuimarisha ushirikishwaji wa wafanyakazi na kuonesha mafanikio katika utekelezaji wa miradi hii ya kimkakati.
Pia ameitaka kusimamia kwa karibu miradi hiyo ili kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kwa uwazi na kutoa matokeo yanayopimika.
“Wizara inawapongezeni kwa kuimarisha ushirikishwaji wa wafanyakazi kupitia Baraza la Wafanyakazi na kuonesha mafanikio katika utekelezaji wa miradi hii ya kimkakati,” amesema Dk Omar.