KAGERA: Walimu walioko kazini pamoja na vijana ambao hawakupata fursa ya kuendelea na elimu ya juu wametakiwa kutumia vyuo vinavyotoa elimu ya ujuzi kwa njia ya masafa ili kujiendeleza na kupata maarifa yatakayowasaidia kukabiliana na mabadiliko ya mfumo mpya wa elimu nchini.

Wito huo umetolewa wakati wa mahafali ya nne ya wahitimu wa Chuo cha DC Polytechnic Education Institute College kilichopo Halmashauri ya Bukoba mkoani Kagera, ambapo jumla ya wanafunzi 908 walihitimu katika ngazi za shahada na astashahada katika fani za ualimu, utawala, uongozi, mawasiliano, teknolojia na ufundi.

Akizungumza katika Kongamano la Wahitimu la chuo hicho, Mkurugenzi wa Huduma za Jamii kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Elieth Lulu Niwagila, alisema maboresho ya mtaala wa elimu yanayotekelezwa na serikali yanalenga kuzalisha wahitimu wenye umahiri, ubunifu na uwezo wa kujitegemea kupitia elimu inayojumuisha maarifa ya vitendo na stadi za kazi.

Alisema mfumo mpya wa elimu unalenga kutoa elimu ya msingi na awali kwa kipindi cha miaka 10 huku ukiweka mkazo katika mafunzo ya amali, ufundi stadi na ujuzi wa kujiajiri.

“Dunia imebadilika sana. Kinachohitajika sasa ni ujuzi. Serikali imeamua kuimarisha elimu inayomjengea mwanafunzi uwezo wa kujitegemea. Hivyo walimu walioko kazini wanapaswa kujiendeleza ili waweze kwenda sambamba na mabadiliko hayo,” alisema Dk. Niwagila.

Aidha, alisema wataalamu wa elimu wamejiridhisha kuwa maboresho ya mtaala yataongeza uwezo wa wanafunzi kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake, Meneja wa DC Polytechnic Education Institute College, Jackson Kailanga, alisema chuo hicho kimejikita katika kutoa elimu inayozingatia mahitaji ya sasa ya soko la ajira na maboresho ya mtaala yanayotekelezwa kupitia Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 pamoja na maboresho yake ya mwaka 2023.

Alisema chuo hicho kinatoa fursa kwa walimu walioko kazini kujiendeleza kielimu kupitia mfumo wa masafa, huku kikianzisha vituo vya mafunzo katika maeneo mbalimbali ili kuwawezesha walimu kupata elimu bila kuathiri majukumu yao ya kazi.

“Tunawaunganisha walimu walioko katika maeneo mbalimbali na kuwafikishia wataalamu kwa ajili ya mafunzo. Hii inawasaidia kuongeza maarifa na kujiandaa vyema kwa utekelezaji wa mtaala mpya,” alisema Kailanga.

Aliongeza kuwa chuo hicho pia kinawapokea vijana waliohitimu kuanzia darasa la saba hadi kidato cha nne na kuwapatia mafunzo ya ufundi katika maeneo mbalimbali ikiwemo ufundi wa magari, umeme na taaluma nyingine za kiufundi kwa kushirikiana na wataalamu kutoka vyuo vya VETA.

Kailanga aliwataka vijana kutokata tamaa kutokana na changamoto za ajira, akisisitiza kuwa fursa nyingi za kujiajiri zinapatikana kwa wenye ujuzi na ubunifu.

Naye Mkurugenzi wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) Kanda ya Ziwa, Godfrey Michael, alisema mhitimu bora ni yule anayetumia maarifa aliyoyapata kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

Aliwahimiza wahitimu kutumia elimu waliyoipata kusaidia jamii, kuongeza ujuzi unaohitajika katika mazingira ya sasa ya kazi, kuepuka vitendo vya rushwa na udanganyifu, na kuwa sehemu ya mafanikio ya utekelezaji wa mtaala mpya wa elimu nchini.

“Maarifa mliyopata yawe chachu ya maendeleo katika jamii zenu. Elimu ni nyenzo muhimu ya kuleta mabadiliko ya kweli na kuongeza kasi ya maendeleo ya taifa,” alisema Michael.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *