Dar es Salaam. Katika kuunga mkono juhudi za kitaifa za kuboresha viwango vya utoaji huduma na kutambua ubunifu katika sekta ya maji, Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imetoa mchango wa Sh50 milioni kudhamini hafla ya tuzo za Tanzania Water Service Excellence Awards inayofanyika jijini Arusha kesho, Jumatatu, Februari 23, 2026.

Hatua hiyo ni juhudi za kuiendeleza dhamira yake ya kusimamia rasilimali maji kwa uwajibikaji na kuendeleza matumizi endelevu ya maliasili.

Akizungumza kuelekea hafla hiyo, Makamu wa Rais wa Masuala ya Uendelevu na Mahusiano ya Kampuni, Afrika wa AngloGold Ashanti, Simon Shayo, amesema udhamini huo unaakisi dhamira ya muda mrefu ya kampuni katika kuchangia maendeleo endelevu na usimamizi makini wa rasilimali.

“Maji ni rasilimali muhimu kwa ukuaji wa uchumi, maendeleo ya viwanda na ustawi wa jamii. Usimamizi bora wa rasilimali hii una athari ya moja kwa moja kwa uimara wa biashara na maendeleo ya taifa kwa ujumla.

  • Kituo cha kusafisha maji kikiwa sehemu ya Mradi wa Maji wa Geita, unaotekelezwa na Kampuni ya Uchumbaji Madini ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa ushirikiano na Serikali. Mradi huo umeongeza upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa Geita kutoka asilimia 3 hadi asilimia 70.

“Kwa kuunga mkono tuzo hizi, tunasisitiza umuhimu wa kuimarisha uongozi na uwajibikaji katika utoaji wa huduma za maji ili kulinda mustakabali wa kiuchumi na kijamii wa nchi yetu,” amesema Shayo.

Ikumbukwe kuwa tuzo hizo ni sehemu ya Mkutano wa Kitaifa wa Mabaraza ya Wakurugenzi wa Mamlaka za Maji Safi na Usafi wa Mazingira (WSSAs), unaoandaliwa na Wizara ya Maji kuanzia kesho, Jumatatu, Februari 23 hadi 25, 2026.

Zaidi ya washiriki 1,000 wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo wenye lengo la kuimarisha uongozi, uwajibikaji na usimamizi bora katika mamlaka zinazohusika na utoaji wa huduma za maji nchini.

Kwa miaka iliyopita, GGML imetekeleza miradi ya maji mkoani Geita, ikiwemo kuchangia Mradi wa Maji wa Geita uliowezesha zaidi ya wananchi 300,000 kupata huduma ya maji safi na salama, pamoja na kuboresha miundombinu ya usambazaji wa maji katika maeneo yanayozunguka mgodi.

Kwa upande wake, Dk Kiva Mvungi, Meneja Mwandamizi wa Afya, Usalama na Mazingira wa GGML, amebainisha kuwa usimamizi endelevu wa maji ni sehemu muhimu ya mikakati ya uendeshaji wa kampuni na mchango wake kwa jamii.

“Kama kampuni ya uchimbaji madini, tunatambua wajibu wetu katika kulinda na kutumia rasilimali maji kwa uangalifu mkubwa. Zaidi ya kutimiza matakwa ya kisheria, tunaendelea kuunga mkono mifumo inayoboresha upatikanaji wa maji kwa muda mrefu na kuimarisha uaminifu wa huduma kwa jamii. Ushirikiano unaoimarisha utawala bora katika sekta ya maji ni nguzo ya maendeleo endelevu,” amesema.

Hata hivyo, upatikanaji wa maji safi na salama unaendelea kuwa kipaumbele katika ajenda ya maendeleo ya Tanzania. Kupitia udhamini huo, GGML inaungana na juhudi za kitaifa za kuboresha viwango vya utoaji huduma na kutambua ubunifu katika sekta ya maji, kwa lengo la kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora na endelevu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *