KATAVI: Zaidi ya wananchi 850 waliokuwa wakisumbuliwa na maradhi mbalimbali wamepatiwa huduma za matibabu na uchunguzi wa afya bila malipo kupitia kambi maalumu ya afya iliyoendeshwa na Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Empower Society Build the Nation (ESBN) mkoani Katavi.

Kambi hiyo ya siku saba imehitimishwa jana baada ya kutoa huduma mbalimbali za kibingwa ikiwemo uchunguzi wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza na ya kuambukiza, matibabu ya macho, upimaji wa virusi vya UKIMWI, uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi na matiti pamoja na ushauri wa afya.

Akizungumza kuhusu mwenendo wa zoezi hilo, Daktari Kiongozi wa timu ya madaktari bingwa wa ESBN, Dkt. Seif Nassor, amewataka wananchi kuweka utaratibu wa kupima afya zao mara kwa mara ili kugundua magonjwa mapema na kupata matibabu kwa wakati.

Amesema magonjwa mengi yasiyo ya kuambukiza, hususan shinikizo la damu, yanachangiwa na mtindo wa maisha usiozingatia afya.

“Maisha ya binadamu kwa ujumla, unakuta upande wa vyakula tunatumia mafuta kwa wingi ambayo yana kiwango kikubwa cha cholesterol, pia tunatumia chumvi nyingi kwenye vyakula vyetu, jambo ambalo husababisha kupanda kwa presha, watu wengi hawafanyi mazoezi wanakula, wanashiba na kulala bila kutenga muda wa kufanya mazoezi. Hali hiyo pia inachangia ongezeko la presha,” amesema Dk. Nassor.

Aidha, amesema kutokunywa maji ya kutosha ni changamoto nyingine inayochangia matatizo mbalimbali ya afya huku akitoa wito kwa wananchi kutumia fursa za kambi za afya zinazoratibiwa na taasisi mbalimbali ili kupata uchunguzi na ushauri wa kitaalamu kabla ya matatizo ya afya kuwa makubwa.

Kwa upande wake, Daktari Hidaya Simba amesema zoezi hilo limefanikiwa kutokana na mwitikio mkubwa wa wananchi waliojitokeza kupata huduma hizo.

Amesema wanaume wenye umri wa miaka 45 na kuendelea wanapaswa kuweka utaratibu wa kupima afya ya tezi dume mara kwa mara ili kutambua mapema viashiria vya ugonjwa huo na kuanza matibabu kwa wakati.

“Tatizo la tezi dume halihusiani na imani za kishirikina kama ambavyo baadhi ya watu wanaamini, haya ni matatizo ya kiafya yanayoweza kumpata mwanaume yeyote anapoendelea kuzeeka, hivyo ni muhimu kufanyiwa uchunguzi wa mara kwa mara,” amesema Dkt. Simba.

Mbali na huduma za afya, ESBN ilihitimisha kambi hiyo kwa kushiriki chakula cha mchana na watoto wanaolelewa katika Kituo cha Mtakatifu Paul II kilichopo Manispaa ya Mpanda, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Mtoto wa Afrika.

Baadhi ya wananchi waliojitokeza katika kambi hiyo wamesema huduma za matibabu na uchunguzi wa afya zilizotolewa zimewasaidia kupata fursa ya kufahamu hali zao za kiafya na kupata ushauri wa wataalamu huku wakiishukuru taasisi hiyo kwa kupeleka huduma hizo mkoani Katavi na kuomba kambi za afya ziwe endelevu ili kuwafikia wananchi wengi zaidi wanaohitaji huduma za kibingwa.

Daudi Madulu, mkazi wa Kijiji cha Kamakuka, amesema aliamua kufika katika kambi hiyo kutokana na huduma kutolewa bila malipo, jambo lililompa nafasi ya kufanyiwa uchunguzi wa afya ambao angeweza kushindwa kuupata kwa urahisi kutokana na gharama.

Naye Mohamed Ramadhan, mkazi wa Manispaa ya Mpanda, amesema alijitokeza kwa hiari yake kupima afya ili kubaini chanzo cha tatizo la macho lililokuwa likimsumbua kwa muda mrefu.

“Nimekuja kupima afya yangu ili kujua tatizo la macho linalonisumbua, mara kadhaa nilikuwa natumia dawa bila ushauri wa daktari, lakini kupitia kambi hii nimepata uchunguzi na ushauri wa kitaalamu ambao utanisaidia kupata matibabu sahihi,” amesema Mohamed.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *