
Dar es Salaam. Timu ya Singida Black Stars imeibuka na ushindi wa mabao 3-1, dhidi ya Mtibwa Sugar, katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, ikikisogeza kikosi hicho hadi nafasi ya 10 kutoka ile ya 13.
Katika mechi hiyo, mabao ya Singida yalifungwa na Mrundi Mossi Nduwumwe, dakika ya tano baada ya piga nikupige lango la Mtibwa Sugar, huku Malanga Mwaku, akifunga la pili dakika ya 17, akiunganisha mpira wa kona uliopigwa na Ibrahim Imoro.
Mabao hayo, yaliiamsha Mtibwa katika kipindi cha pili, ingawa umakini mbovu wa safu ya kujilinda ulionekana, baada ya kuruhusu bao la tatu lililofungwa kwa kichwa na beki, Kennedy Juma dakika ya 53, akimalizia kona ya Ande Koffi Cirille.
Hata hivyo, jitihada za Mtibwa Sugar mwishoni mwa mechi hiyo, zilizaa matunda baada ya mshambuliaji wa kikosi hicho, Raizin Hafidh kufunga bao la kufutia machozi dakika ya 88, akimaliza krosi iliyopigwa na beki wa kulia, Datius Peter.
Ushindi huo kwa Singida unaifanya timu hiyo kusogea hadi nafasi ya 10 katika msimamo wa Ligi Kuu, baada ya kufikisha pointi 15, ambazo ni sawa na za Coastal Union iliyosogea nafasi ya 11 kutoka ile ya 10, kufuatia kucheza mechi tisa.
Kwa upande wa Mtibwa, kichapo hicho ni cha pili mfululizo kwa Kocha, Mkenya Yusuf Chippo, tangu ajiunge nayo, baada ya mechi iliyopita dhidi ya Mashujaa iliyopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma kuchapwa pia mabao 3-1, Februari 13, 2026.
Kichapo hicho cha Mtibwa ni cha pili kwa Chippo Ligi Kuu Bara tangu alipojiunga na timu hiyo, Novemba 17, 2025, ambapo kabla ya hapo aliiongoza kwenye mechi nane bila ya kupoteza, huku kati ya hizo akishinda nne tu na kutoka sare pia nne.
Chippo aliyewahi kuzifundisha timu mbalimbali zikiwemo za Pamba Jiji, Coastal Union na TRA United zamani Tabora United, alijiunga na kikosi hicho Novemba 17, 2025, baada ya kuachana na Murang’a SEAL ya kwao Kenya tangu, Agosti 21, 2025.
Kwa matokeo hayo, Mtibwa inaendelea kubakia katika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu na pointi 21, baada ya timu hiyo kushinda mechi tano, sare sita na kupoteza minne kati ya 15, iliyocheza, ikifunga mabao 13, huku ikiruhusu pia 14.