Dar es Salaam. Makamishina 13 wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa) wamevalishwa vyeo, wakisisitizwa kufanya kazi kwa kushirikiana ili kutengeneza mazingira rafiki ya kufanyia kazi na kutimiza majukumu yao ya kila siku kwa weledi.
Hafla hiyo imefanyika jana, Jumamosi Februari 21, 2026 katika ofisi za Tawa na kuhudhuriwa na maofisa waandamizi wa mamlaka hiyo.
“Ni vema mkatumia nafasi zenu kufanya kazi kwa kushirikiana huku mkitumia ujuzi wenu mliopata kuhakikisha Tawa inapaa na kuongeza fursa za utalii na uwekezaji,” amesema Meja Jenerali mstaafu, Hamis Semfuko, baada ya kuwavisha vyeo hivyo.
Amesema makamishna waliovishwa vyeo wakatekeleze maelekezo ya Serikali na maono ya Bodi ya Wakurugenzi ya Tawa kuhakikisha mamlaka hiyo inakuwa na viwango.
Katika hafla hiyo, Kaimu Kamishna wa Uhifadhi, Mlage Kabange amesisitiza umuhimu wa kutumia rasilimali zilizopo kukamilisha majukumu yao ya kila siku na kuleta tija kwenye maeneo yao ya kazi.
Meja Jenerali Mstaafu Hamis Semfuko akiwavisha rasmi vyeo vipya makamishina waliopandishwa vyeo. Kushoto kwake ni Kaimu Kamishna wa Uhifadhi, Mlage Yussuf Kabange.
Amesema kiongozi bora anapimwa kwa kutumia ‘resources’ kidogo zilizopo kufanya kazi yenye ufanisi, kwa sababu changamoto ya rasilimali haziwezi kutatuliwa kwa asilimia 100.
Naibu Kamishna wa Uhifadhi anayeshugulikia Kurugenzi ya Huduma za Shirika,Maarufu Mkwaya katika siku za hivi karibuni mamlaka hiyo imepata askari wapya 296.
Mkwaya amesema askari hao wanaenda kuongeza tija kwenye utendaji kazi wa mamlaka na kwamba viongozi waliovalishwa na kupandishwa vyeo wanakwenda kwenye ngazi za kanda, kwa maana ya viongozi wa kanda za Tawa.