Dar es Salaam. Unakumbuka ‘sindano’ iliyomchoma aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), hayati Maalim Seif Sharif Hamad na kumuondoa katika chama hicho, alichokitumikia muda mrefu na kutimkia ACT-Wazalendo kuendeleza siasa?

Basi, sindano hiyo, ndiyo iliyomchoma Profesa Ibrahim Lipumba, aliyejikuta nje ya uongozi wa chama hicho, baada ya kukiongoza kwa takriban miongo mitatu kwa wadhifa wa uenyekiti wa Taifa.

Maalim Seif anayezungumziwa hapa si yule aliyekuwa ACT-Wazalendo, bali wa ‘Ngunguli na Ngangari’ akiwa kada mtiifu wa CUF akiitumikia kwa sehemu kubwa ya ujana wake.

Utumishi wake ndani ya chama hicho, cha pili kwa ukongwe nchini baada ya Chama cha Mapinduzi (CCM), ukamjengea umaarufu kiasi cha kupewa majina kama ‘Rais wa Watu.’

Lakini, juhudi zote na utumishi wake ndani ya CUF, zilikoma mwaka 2019. Alitangaza kukihama chama hicho baada ya kuibuka mgogoro wa uongozi uliotokana na Profesa Lipumba kutangaza kujiuzulu uenyekiti lakini ghafla akarejea kwenye nafasi hiyo.

Uamuzi wa Profesa Lipumba ulizua tafrani ndani ya chama hicho, maswali yakaibuka, iweje mchumi huyo arejee ghafla, wakati tayari chama kilishakuwa chini ya Maalim Seif.

Hivyo, uamuzi wa Profesa Lipumba kurejea ndani ya chama hicho kwa nafasi ya uenyekiti aliyojiuzulu miezi kadhaa iliyopita, ukabarikiwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kuanzia hapo CUF haikuwahi kukaa sawa.

Maalim Seif hakuridhika, akaitafuta haki kupitia muhimili wa Mahakama.

Alifungua kesi Mahakama Kuu kupinga hatua ya Profesa Lipumba kurejea madarakani. Hata hivyo, ushindi haukuwa upande wake.

Mwanasiasa huyo hakukata rufaa kwa kwenda Mahakama ya juu zaidi, alikatia rufaa uanachama wake wa CUF na kutangaza kujiunga na jukwaa jipya la ACT- Wazalendo, akiwa na kundi lililokuwa likimuunga mkono, hiyo ilikuwa mwaka 2019.

Zamu ya Profesa Lipumba

Hata hivyo, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa iliyobariki kurejea kwa Profesa Lipumba madarakani mwaka 2019, imesema mwaka 2024 alichaguliwa katika mazingira batili.

Baadhi ya wanachama waliandika barua kwa msajili wakilalamikia ushindi wake, wakisema alipata kura pungufu.

Hakukuwa na majibu yaliyopatikana kutoka katika ofisi hiyo inayoshughulika na ulezi wa vyama, hadi miaka miwili baadaye. 

Februari 13, 2026 Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi alitengua uchaguzi wa mwaka 2024 uliomweka madarakani Profesa Lipumba na wenzake watano.

Viongozi wengine watano waliathirika na utenguzi huo ni Makamu Mwenyekiti (Zanzibar) Mbarouk Seif Salim, Makamu Mwenyekiti (Tanzania Bara) Othman Dunga, Katibu Mkuu Husna Mohamed Abdallah, Naibu Katibu Mkuu Magdalena Sakaya (Tanzania Bara) na Ali Juma Khamis (Zanzibar).

Sababu ya kutenguliwa kwa uchaguzi huo uliofanyika Desemba 18 na 19, 2024, ni kwamba Profesa Lipumba na wenzake hawakupata ushindi wa zaidi ya nusu ya kura halali zilizopigwa.

Kwa mujibu wa katiba ya chama chao, matokeo hayo yalipaswa kusababisha uchaguzi urudiwe.

Hali hiyo imekigawa chama hicho katika makundi mawili, kundi la Profesa Lipumba linalodai litapinga uamuzi wa msajili mahakamani, likisema haukuzingatia haki yao ya msingi ya kusikilizwa kabla ya uamuzi kufanyika.

Kundi lingine, linawahusu wanachama wanaounga mkono uamuzi huo wakiwamo waliowasilisha malalamiko dhidi ya uchaguzi wakidai ulikuwa na dosari nyingi.

Lipumba ang’oka

Februari 21, 2026, ilikuwa siku ya Mkutano Mkuu wa chama hicho, wajumbe kutoka mikoa mbalimbali walikutana kwa lengo la kufanya uamuzi wa uongozi.

Katika mkutano huo, Profesa Lipumba na safu yake ya juu waliondolewa madarakani.

Mkutano huo uliofanyika katika Ukumbi wa Lekham, Buguruni, mkabala na makao makuu ya chama, ulitawaliwa na shamrashamra, kejeli na malumbano, hasa baada ya baadhi ya wafuasi wa Lipumba kuamua kuchukua fomu za kugombea wakidai kuwa, huwezi kupinga jambo ukiwa nje ya mfumo.

Kabla ya mkutano huo, kulikuwa na mchujo wa wagombea wa nafasi za uenyekiti Taifa, makamu mwenyekiti Tanzania Bara na makamu mwenyekiti Zanzibar.

Mkutano huo uligubikwa na matukio ya kushangaza kuanzia kwa wajumbe wa mkutano mkuu hadi wale wa baraza kuu la chama.

Mambo mengi yaliendeshwa kwa haraka, kana kwamba ni mkutano wa zimamoto.

Wajumbe wengi walivaa kofia zenye picha ya Maalim Seif Sharif Hamad, wakidai kuwa enzi za uongozi wa Profesa Lipumba zimefikia tamati na sasa ni zama mpya.

Baadhi ya wajumbe, akiwamo Mohammed Nassor walinukuliwa wakisema sasa ni wakati wao kunufaika na matunda ya chama na kwamba waliokuwa wakinufaika awali ni zamu yao sasa kupitia kipindi cha changamoto.

Nassor amesema Profesa Lipumba alikuwa tayari kuachia wadhifa huo, lakini washauri wake wa karibu walimtaka aendelee kutokana na manufaa waliyokuwa wakiyapata chini ya uongozi wake.

Kwa upande wa wafuasi wa Profesa Lipumba, Rashid Hussein amenukuliwa akidai kuwa chama kinaelekea kuporomoka kwa sababu kundi linalochukua uongozi halina dhamira njema bali linafuata masilahi binafsi.

Kutokana na hali hiyo, taswira iliyojitokeza ni kwamba mchakato huo haukuwa tu uchaguzi wa kidemokrasia, bali pia ulikuwa na sura ya kushughulikia tofauti za makundi.

Baadaye, wagombea watatu kwa kila nafasi walipitishwa na kikao cha dharura kilichofanyika asubuhi ya siku hiyo.

Kwa nafasi ya uenyekiti Taifa, wagombea walikuwa Mirambo Yusuf aliyeibuka mshindi dhidi ya Othman Dunga na Ntimwinyilike Siwale.

Katika hatua ya kujinadi, makundi ya Profesa Lipumba na Maalim Seif yalionekana kujikita zaidi katika misimamo ya kimakundi badala ya kuwasilisha sera mbadala kwa uwazi.

Maswali yaliyoulizwa kwa wagombea yalielemea zaidi katika mvutano wa makundi kuliko hoja za sera na mustakabali wa chama.

Wajumbe wengi walionekana kuwa na dhamira ya kutimiza azma ya kuiondoa safu ya Profesa Lipumba madarakani.

Hata hivyo, katika hatua ya mapumziko ya futari, kulizuka malalamiko kutoka kwa baadhi ya wanachama waliodai kuwa, haikuwa busara kuendelea na mkutano ilhali wengi wao walikuwa na njaa, jambo lililoongeza taharuki katika mkutano huo.

Mkutano kusimama

Ilipofika saa moja kamili usiku, mkutano huo ulisimama kwa takribani saa moja ili kupisha wajumbe kwenda kupata futari.

Baadaye walirejea kuendelea na mchakato wa kuwasikiliza wagombea na kuwauliza maswali.

Wajumbe wa kikao cha Baraza Kuu la Chama cha Wananchi (CUF) wakiwa katika kikao hicho kinachoendelea makao makuu ya Chama hicho Buguruni, Dar es Salaam.

Mchakato uliendelea huku mijadala ya kisiasa ikishika kasi, hali iliyomlazimu msimamizi wa uchaguzi kutoa onyo kutokana na hekaheka za kuingia na kutoka zilikuwa zimezidi, jambo lililoweza kuhatarisha usalama wa mchakato huo kwa kuruhusu mamluki kuingia.

Kuanzia saa tatu na nusu usiku, shughuli ya kupiga kura ilianza. Ilipofika saa 4:24 usiku, mkutano huo ambao haukuhudhuriwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, tofauti na ilivyo kwa mikutano mingine ya vyama ulikuwa umekamilisha upigaji kura, huku wajumbe wakijadiliana namna ya kuhesabu kura za wagombea.

Baadaye, wamiliki wa ukumbi walifika na kuwataka waondoke, wakidai kuwa muda waliokubaliana wa kutumia ukumbi ulikuwa umeisha. Walitishia kuzima umeme ili kupisha shughuli nyingine.

Hatua hiyo ililazimu Jeshi la Polisi, ambalo lilikuwa limezingira ukumbi huo kuimarisha ulinzi, kuongeza tahadhari katika kila kona wakati wagombea na mawakala wao wakifungasha masanduku ya kura, yaliyofungwa kwa bendera ya chama husika, kwa ajili ya kupelekwa makao makuu ya chama kwa kuhesabiwa.

Hatua hiyo ilisababisha usumbufu mkubwa. Wajumbe walilazimika kutoka ukumbini kwa miguu kuelekea makao makuu ya chama hicho kusubiri matokeo.

Shughuli ya kuhesabu kura ilianza saa 5:17 usiku na kumalizika saa 6:06 usiku.

Baada ya majumuisho kufanyika, alipatikana mrithi wa Profesa Lipumba, ambaye ni Mirambo Yusuf, atakayekiongoza chama hicho kwa miaka mitano ijayo. Mirambo alipata kura 256 na kumshinda mpinzani wake, Othman Dunga, aliyepata kura 177.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *