Mwanza. CRDB Bank Foundation imesaini mkataba wa ushirikiano na Kafiti Foundation kwa lengo la kuwawezesha kiuchumi vijana na wanawake wajasiriamali katika Jimbo la Ilemela, mkoani Mwanza. Hafla ya utiaji saini ilifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita sambamba na mahafali ya wahitimu 461 waliopata mafunzo katika Chuo cha Ufundi Stadi (Veta) Ilemela.
Ushirikiano huo umeanza kwa kutoa mafunzo kwa madereva wa bodaboda na bajaji, yakihusisha elimu ya ujasiriamali, usimamizi wa fedha na upatikanaji wa mitaji wezeshi. Lengo ni kuwajengea uwezo wa kujitegemea na kuinua kipato chao kupitia shughuli halali za kiuchumi.
Akizindua programu hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, amesema zaidi ya madereva 5,000 wanatarajiwa kunufaika kupitia awamu 11 za mafunzo. Amepongeza ubunifu wa mpango huo, akieleza kuwa ni mara ya kwanza kushuhudia mpango maalumu wa kuwawezesha madereva wa bodaboda kwa ushirikiano wa sekta binafsi.
Katika utekelezaji wake, vijana watanufaika na mikopo nafuu ikiwemo pikipiki 12,000 pamoja na ujenzi wa vituo vya kuchaji pikipiki za umeme Jimbo la Ilemela ili kupunguza gharama za uendeshaji. Wanawake wajasiriamali pia watapatiwa mafunzo ya ujasiriamali na elimu ya fedha.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kafiti Foundation, Mhandisi Mapuri William, amesema taasisi hiyo inalenga kupunguza umaskini kwa kuwawezesha vijana kujitegemea. Mbunge wa Ilemela, Kafiti William Kafiti, amesema wahitimu walilipiwa ada na gharama za leseni, huku wakichangia Sh20,000 kati ya Sh70,000 zilizohitajika na salio likitolewa kama mkopo utakaorejeshwa kwa awamu.
Kwa upande wake, Meneja Mafunzo na Uwezeshaji wa CRDB Bank Foundation, Joshua Mwakalobo, amesema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kufungua fursa za kiuchumi kwa vijana na wanawake nchini.