Dar es Salaam. Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Jude Thaddaeus Ruwa’ichi ametangaza ratiba ya mazishi ya aliyekuwa Askofu Mkuu wa Jimbo hilo, Polycarp Kardinali Pengo huku baadhi ya viongozi wakimtaja kama kiongozi wa kiroho aliyekuwa daraja la maelewano na mshauri mwenye busara katika masuala ya kitaifa.
Ruwa’ichi ametangaza ratiba hiyo akisisitiza kifo chake ni pengo kubwa kwa Kanisa na Taifa kwa ujumla.
Ratiba hiyo imetangazwa rasmi, huku waumini wa Kanisa Katoliki na Watanzania kwa ujumla wakialikwa kushiriki ibada na shughuli za kumuaga kiongozi huyo wa kiroho aliyefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Akizungumza katika Kanisa Kuu la St. Joseph, jijini Dar es Salaam, leo Jumatatu, Februari 23, 2026 Askofu Mkuu Ruwa’ichi amesema Kardinali Pengo atazikwa Jumamosi, Februari 28, katika makaburi ya Pugu, eneo aliloliandaa mwenyewe miaka michache iliyopita na kuonesha nia ya kutaka kuzikwa huko.
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Judde Thaddaeus Ruwa’ichi akizungumza na waandishi wa habari juu ya taarifa rasmi ya maziko ya Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, leo Februari 23, 2026 katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu Jimbo Kuu la Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, Ijumaa Februari 27, mwili wa marehemu utachukuliwa kutoka Lugalo Mortuary na kuletwa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph (St Joseph Cathedral) kuanzia saa 3 asubuhi, ambapo waumini na wananchi watapata nafasi ya kutoa heshima za mwisho.
“Misa takatifu ya kumuombea itaanza saa 7 mchana, na baada ya misa hiyo waombolezaji wataendelea kutoa heshima hadi saa 10 jioni, ambapo itaadhimishwa misa nyingine. Baada ya hapo, mwili utabaki kanisani kwa ajili ya ibada ya mkesha kwa watakaopenda kukesha wakisali na kuimba,” amesema Ruwa’ichi.
Amesema Jumamosi ya Februari 28, saa 12 alfajiri, mwili utaondolewa Kanisa Kuu la St Joseph na kupelekwa Pugu, ambako misa ya mazishi itaanza saa 4 asubuhi.
Askofu Mkuu Ruwa’ichi amesema amepokea msiba huo kwa imani, akimuomba Mungu amjalie marehemu pumziko la milele, na kuwataka waumini na watu wote wenye mapenzi mema kujitokeza kwa wingi kushiriki ibada na mazishi hayo.
Maisha na utume wake
Akizungumzia maisha ya marehemu, Askofu Mkuu Ruwa’ichi amesema Kardinali Pengo alijitambulisha kimataifa kama kiongozi wa kanisa aliyejituma kuitangaza Injili kwa mapana na marefu.
Ameeleza Kardinali Pengo alipata elimu ya juu Roma na kutunukiwa Shahada ya Udaktari mwaka 1976, kabla ya kurejea nchini na kufundisha katika Seminari ya Kipalapala. Ruwa’ichi amesema alimfahamu kama mwalimu wake na baadaye kushirikiana naye katika utumishi wa kanisa.
“Aliporudi nyumbani akaenda kufundisha seminari ya Kipalapala, mimi nikiwa mwanafunzi katika mwaka wake wa kwanza kama mwalimu, alikuwa mwalimu wangu na mzuri, nashukuru Mungu kwamba nilimfahamu na amenifundisha na pia nimefanya naye kazi,” amemwelezea.
Kwa mujibu wa Askofu Mkuu huyo, Kardinali Pengo aliongoza Jimbo Kuu la Dar es Salaam kwa mafanikio makubwa, akilikuza kutoka parokia 20 alizozikuta hadi kufikia parokia 105 alizomkabidhi mwaka 2019.
Katika kipindi chake cha uongozi, aliratibu pia shughuli za majimbo yaliyo chini ya Kanda ya Dar es Salaam, yakiwemo Mahenge, Ifakara, Zanzibar, Tanga na Bagamoyo, akihakikisha ushirikiano na uratibu wa kichungaji unaimarika.
Changamoto za kiafya
Kuhusu sababu ya kifo chake, amesema Kardinali Pengo alikuwa na changamoto za kiafya kwa muda mrefu, ikiwemo ugonjwa wa moyo uliomlazimu kufanyiwa upasuaji na kuwekewa kifaa cha kusaidia mapigo ya moyo (pacemaker).
Askofu Mkuu mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Polycarp Kardinali Pengo. Picha na Mtandao
Aidha, aliwahi kufanyiwa upasuaji wa uti wa mgongo nchini Ujerumani, India na baadaye Marekani katika Hospitali ya Cornell, ambapo alifanyiwa upasuaji mkubwa uliodumu kwa saa 13.
Amesema upasuaji huo ulimsaidia kurekebisha tatizo la kupinda kwa mgongo na kurejea katika hali ya kutembea wima kabla ya kuendelea na majukumu yake hadi alipofariki dunia.
Wito wa kuendelea kumuombea
Naye Paroko wa Kanisa Kuu la St Joseph, Padre Denis Mwingira, amewataka waumini na wananchi kuendelea kumuombea marehemu na kumshukuru Mungu kwa maisha na utumishi wake.
Padre Mwingira amesema alimfahamu Kardinali Pengo kama mchungaji mwerevu, mpole na mwenye kujishusha, aliyeishi maisha ya kawaida licha ya nafasi yake kubwa ndani ya kanisa.
“Yeye ndiye aliyenikubali nifike hatua ya upadre, ninamfahamu kama padre kwa maana alinichagua pia kuwa Katibu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam na pia niliwahi kuwa dereva wake wakati wa uongozi wake.”
“Kwa hiyo nimemfahamu kama mchungaji, mwerevu, mpole na mwenye kujishusha na wakati namwendesha hakuwa na shida yoyote hivyo sikuwa na hofu ya kuendesha kwa woga,” amemwelezea.
Spika wa Bunge la Tanzania, Mussa Azzan Zungu akisaini kitabu cha maombolezo ya Askofu Mkuu mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Polycarp Kardinali Pengo leo Jumatatu, Februari 23, 2026 kwenye viwanja vya Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu jijini Dar es Salaam. Picha na Herieth Makwetta
Amesema marehemu alikuwa na upendo wa pekee kwa Yesu wa Ekaristi, akiamini huo ndio chanzo na kilele cha utumishi wa kikuhani, na kwamba urithi wake mkubwa ni ushuhuda wa maisha ya sala, unyenyekevu na uaminifu katika kuhubiri injili.
Viongozi wamzungumzia
Baadhi ya viongozi wametembelea na kuweka saini katika kitabu cha maombolezo akiwemo Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu na Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir.
Akimzungumzia, Mufti Zubeir amesema kifo cha Kardinali Pengo ni pigo kwa Taifa, akimtaja kama kiongozi wa kiroho aliyekuwa daraja la maelewano na mshauri mwenye busara katika masuala ya kitaifa.
Amesema alifahamiana na Kardinali Pengo kwa muda mrefu na tangu alipoingia katika Baraza kama Mufti, waliendelea kushirikiana kwa karibu wakijadili masuala yenye masilahi mapana ya nchi.
“Hayati Pengo ni mzee wetu ambaye tumeishi naye vizuri katika kipindi chote. Tangu nimeingia katika Baraza kama Mufti nimeendelea kushirikiana naye vizuri. Tulikuwa tukizungumza masuala yenye masilahi ya nchi, alikuwa mtu wa ushauri na kila ukizungumza naye ulikuwa hupati neno tu bali faida,” amesema.
Amesema Taifa limeondokewa na mtu muhimu, lakini akaeleza kuwa mapenzi ya Mungu ni makuu na maisha ya duniani ni ya kupita.
“Tunaweza kusema tumeondokewa na mtu muhimu katika nchi, lakini yote ni mapenzi ya Mungu hapa duniani ni mahali pa kupita tu na si mahali pa kukaa,” amesema.
Mufti huyo amemwelezea Kardinali Pengo kama kiongozi mwenye utulivu na hekima, aliyekuwa na uwezo wa kutuliza mambo pale yanapokuwa mazito au yenye mvutano.
“Kama kuna jambo zito, alikuwa analituliza. Alikuwa anakaa na kila mtu, mnyonge na asiye na uwezo. Hiyo ilikuwa sifa yake kubwa,” amesema.
Akikumbuka moja ya matukio waliyoshiriki pamoja, Muft Zubeir amesema waliwahi kukaa pamoja wakati wa hafla ya kuapishwa kwa Rais katika Uwanja wa Taifa, akieleza jinsi Kardinali Pengo alivyoonesha ukarimu na unyenyekevu hata katika mazingira ya ulinzi mkali.
“Alipokuwa anaapishwa Rais pale Uwanja wa Taifa, tulikuwa mimi na yeye pamoja. Kulikuwa na wakati nataka kwenda kujitengeneza mahali, akamwambia mlinzi wake anisindikize. Hata katika mazingira yale, alionesha ukarimu na utu wake,” amesimulia.
Amesema wapo katika kipindi cha maombolezo na bado wana mengi ya kusema kuhusu mchango wa marehemu, akiahidi kuendelea kuenzi mema aliyoyaacha.