Unguja. Wakati la kukatika kwa umeme mara kwa mara na kuibua malalamiko kisiwani Zanzibar, Serikali imesema hali hiyo inasababishwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukuaji wa uchumi na kuongezeka kwa idadi ya watu na makazi, hivyo kusababisha njia kuu za umeme kwenda kwa mtumiaji wa mwisho kuzidiwa.

Hivyo, ili kunusuru nyaya kuanguka, inalazimu kuzima umeme baadhi ya maeneo ili kuleta uwiano katika mifumo ya umeme.

Zanzibar inapokea umeme kupitia waya za baharini kutoka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco). Kwa upande wa Unguja, zipo nyaya mbili, moja ya megawati 45 iliyowekwa mwaka 1980 na imetumika hadi kufikia asilimia 98.8 na ya pili ya megawati 100 imetumika kwa asilimia 97.3, ambapo nyaya zote zimeshafikia ukomo wa uwezo wa kusafirisha umeme.

Akizungumza leo Februari 23, 2026 katika mkutano wa pili wa Baraza la 11 la Wawakilishi, Naibu Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Seif Kombo Pandu amesema kwa sasa kisiwa cha Unguja kinapokea megwati 135.7 wakati mahitaji kwa sasa ni megawati 165, hivyo kwa kisiwa cha Unguja kuna nakisi ya mahitaji ya umeme kwa megawati 30.

“Kwa kisiwa cha Pemba tunapokea megawati 20, wakati mahitaji ni megawati 16.7,” amesema.

Majibu hayo yalitokana na swali la Mwakilishi wa Chambani, Mahmoud Shineni Ali (ACT Wazalendo) kuhusu sababu zinazofanya kukatika kwa nishati hiyo mara kwa mara na mpango mkakati wa Serikali wa kuliondosha tatizo hilo ambalo limekuwa likileta hasara kwa wananchi.

Naibu Waziri amesema katika kukabiliana na tatizo la upungufu wa umeme, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Shirika la Umeme Zanzibar, limechukua hatua tofauti ikiwemo kuyawasha majenereta 30 na kuingiza kwenye gridi megawati 20.

Amesema mchakato huo uko katika hatua za mwisho, ambapo kwa sasa Shirika la Umeme linafanya uwiano wa umeme unaotoka katika majenereta hayo na gridi, baada ya kukamilika, tatizo hilo litapungua kwa kiasi kikubwa.

“Aidha Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia shirika la umeme iko katika hatua za mwisho kuingiza megawati 35 katika gridi kutoka katika meli maalum ya kuzalisha umeme iliopo nyuma ya Hoteli ya Verde Mtoni,” amesema

Hata hivyo, amesema upungufu wa umeme uliopo ni janga la bara zima la Afrika, ikiwemo Tanzania, hata katika mkutano wa nishati wa Afrika uliofanyika Februari 2025 jijini Dar es Salaam uliainisha uwepo wa upungufu kwa nishati ya umeme barani Afrika ikiwa ni pamoja na Tanzania na kuazimiwa kuchukua juhudi mbalimbali kukabiliana na upungufu huo.

 “Hivyo, kwa kuwa ni janga la kitaifa na si tukio mahsusi, Serikali kwa sasa haiwezi kufanya tathmini kwa ajili ya fidia kama mheshimiwa mwakilishi anavyotaka kuwapa fidia,” amesema.

Hata hivyo, amesema Serikali imekuwa na mipango madhubuti ya muda wa kati na muda mrefu ilioanza kutekelezwa kupitia miradi inayofadhiliwa na Benki ya Dunia na ile inayofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika kukabiliana na hali hio.

Amesema “baada ya miradi hio kukamilika, tatizo hilo litaondoka.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *