Mwanza. Taasisi inayoshughulika na kuwasaidia watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (watoto njiti) ya Doris Mollel chini ya Mkurugenzi Mtendaji wake, Doris Mollel itajenga majengo maalumu kwa ajili ya kutoa huduma bora kwa watoto hao katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Tabora, Shinyanga, Geita na Zanzibar.
Hatua hiyo inakuja baada ya taasisi hiyo kufanikisha ujenzi wa jengo jipya la kisasa maalumu la kwanza nchini kwa ajili ya kutoa huduma bora kwa watoto hao wanaozaliwa kabla ya wakati lililopo katika Hospitali ya Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.
Jengo hilo lenye thamani ya Sh2.1 bilioni linatarajiwa kuzinduliwa rasmi Februari 28, 2026 na Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus.
Jengo hilo limejengwa kwa ushirikiano na Taasisi ya Msanii wa Marekani, Alicia Keys inayoitwa Keep a Child Alive na ni jengo maalumu kwa kuwa linaenda kuhamasisha mtoto kutotengwa na mama yake na lina chumba maalumu kwa ajili ya baba kumuona mama na mtoto wake akiwa hospitalini hapo, huku likiwa na uwezo wa kuhudumia watoto 42 kwa wakati mmoja.
Muonekano wa ndani wa jengo jipya la kisasa maalum kwa ajili ya kutoa huduma bora kwa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati lililopo katika Hospitali ya Wilaya ya Kwimba Mkoani Mwanza.
Hayo yanafanyika wakati takwimu zikionesha kuwa takribani asilimia 11 ya watoto wanaozaliwa Tanzania huzaliwa kabla ya wakati (njiti) na zaidi ya asilimia 30 ya vifo vya watoto wachanga vinahusishwa moja kwa moja na matatizo ya kuzaliwa kabla ya wakati.
Akizungumza leo Jumatatu, Februari 23, 2026 na waandishi wa habari katika Hospitali ya Wilaya Kwimba, mkoani Mwanza, Mkurugenzi huyo amesema ujenzi wa jengo hilo umeenda sambamba na ujenzi wa nyumba mbili za wauguzi ambazo tayari zimekamilika.
“Baada ya kukamilisha ujenzi Kwimba, taasisi itakwenda pia kujenga majengo kama hayo kwenye mikoa mingine ikiwemo Dar es salaam, wilaya tatu za Mwanza, Wilaya mbili za Shinyanga na Geita, Tabora pamoja na Zanzibar ambapo lengo ni kujenga kuzijenga 10 hadi kufikia mwaka 2028,” amesema.
Katika jengo hilo linalotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni, Mkurugenzi huyo ndiye msimamizi mkuu kuanzia wazo, kutafuta wadau na wafadhili akiwemo Alicia Keys pamoja na kufanya juhudi kwa Serikali kutoa wauguzi na hata kumshawishi Dk Tedros kuja kuzindua.