
Waziri wa zamani wa Uingereza na balozi Peter Mandelson amekamatwa siku ya Jumatatu, Februari 23, kama sehemu ya uchunguzi kuhusu uhamisho wa taarifa nyeti kwa mfadhili wa Marekani na mtuhumiwa wa uhalifu wa ngono kwa watoto wadogo, Jeffrey Epstein.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 3 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
“Polisi wamemkamata mwanamume mwenye umri wa miaka 72 kwa tuhuma za kupuuza wajibu wake,” polisi ilisema katika taarifa, bila kufichua utambulisho wa mshukiwa, kama ilivyo kawaida nchini Uingereza.
BBC na Sky News zilionyesha picha za Peter Mandelson, mwenye umri wa miaka 72, akiondoka nyumbani kwake katikati mwa London, akiandamana na mwanamume na mwanamke waliomsindikiza hadi kwenye gari lisilo na namba ya usajili.
Polisi wanamchunguza Peter Mandelson kuhusu hati zinazoonyesha kwamba alimpa Epstein taarifa nyeti za serikali miaka 15 iliyopita. Hashutumiw kwa utovu wa nidhamu wa kingono. Kukamatwa kwake kunakuja siku nne baada ya Andrew Mountbatten-Windsor, mwanamfalme wa zamani Andrew, ambaye anashukiwa kwa kosa kama hilo linalohusiana na urafiki wake na Epstein.
Peter Mandelson alifukuzwa kazi katika wadhifa wake wa kidiplomasia mnamo mwezi Septemba baada ya kuchapishwa kwa barua pepe zilizofichua kwamba alidumisha urafiki na Epstein baada ya hatia ya Epstein mnamo mwaka2008 kwa biashara haramu ya ngono ya watoto. Kufuatia kutolewa kwa maelezo mapya katika hati zilizochapishwa mwezi uliopita na Wizara ya Sheria ya Marekani, polisi ilifungua uchunguzi wa jinai.
Mnamo Februari 6, polisi ilitangaza kwamba ilikuwa ikitafuta makazi mawili ya Mandelson, moja katika kitongoji cha kifahari cha Regent’s Park jijini London na jingine huko Wiltshire. Gordon Brown pia alisema kwamba aliwapa polisi taarifa kuhusu kile alichokielezea kama “kitendo kisicho na udhuru na kisicho cha uzalendo” cha Mandelson. Nyaraka pia kutoka kwa faili za Epstein zinaonyesha kwamba Peter Mandelson alipokea malipo ya jumla ya dola 75,000 (euro 63,200) kutoka kwa mfadhili huyo wa Marekani.
Serikali ya Starmer imedhoofika
Maendeleo haya yameidhoofisha serikali ya Labour ya Keir Starmer, ambayo inashutumiwa kumteua Peter Mandelson kama balozi wa Washington mwishoni mwa mwaka 2024, ingawa alijua kwamba waziri huyo wa zamani na kamishna wa zamani wa Ulaya waliendelea kuwa washirika wa karibu wa Epstein baada ya kupatikana na hatia ya uhalifu wa ngono.
Keir Starmer, ambaye tayari alimrudisha nyumbani Peter Mandelson mnamo mwezi Septemba 2025, aliomba radhi, haswa kwa waathiriwa wa Jeffrey Epstein. Wafanyakazi wengine watatu wa Keir Starmer waliacha nyadhifa zao mnamo mwezi Februari: Chris Wormald, Katibu wa baraza la mawaziri, mtumishi mkuu wa umma nchini anayehusika na kumshauri Waziri Mkuu; mkurugenzi katika ofisi ya waziri mkuu, Morgan McSweeney; na mkurugenzi wa mawasiliano katika ofisi ya Waziri mkuu, Tim Allan.
Serikali tangu wakati huo imeahidi kutoa hati zote zinazohusiana na uteuzi na kufukuzwa kwa Peter Mandelson. Kundi la kwanza linatarajiwa kuchapishwa mapema mwezi Machi, afisa wa serikali alisema siku ya Jumatatu, Februari 23. Kulingana na BBC, hii inajumuisha zaidi ya hati 100,000, ikiwa ni pamoja na barua pepe kati ya balozi wa zamani na wajumbe wa Serikali.
Baadhi ya hati hizi, ambazo zinaweza kuwa nyeti kwa usalama wa taifa, hupitiwa kwanza na kamati ya bunge, ambayo ina uhuru wa kuamua kama itaziweka hadharani au la.
Kampuni ya ushauri iliyoanzishwa na Peter Mandelson, Global Counsel, ambayo biashara yake iliathiriwa sana na ufichuzi kuhusu uhusiano wa mtendaji huyo wa zamani na mtuhumiwa wa uhalifu wa ngono kwa watoto wadogo Jeffrey Epstein, iliwekwa chini ya utawala wa mahakma, wasimamizi wake wapya walitangaza siku ya Ijumaa, Februari 20.
“Sasa tutafanya mapitio ya kina ya mali na madeni ya kampuni na kuchunguza njia bora ya kufikia [kuuza] mali zake,” Will Wright, mkurugenzi mkuu wa shirika la ushauri wa marekebisho la Interpath, ambaye aliteuliwa kuwa msimamizi mwenza, alisema katika taarifa.
Global Counsel, kampuni ya mawasiliano na mahusiano ya umma, ilitangaza nia yake ya kuwasilisha maombi ya utawala, ikitaja “mzozo unaoendelea wa umakini wa kisiasa na vyombo vya habari unaomzunguka Peter Mandelson, ambao umefanya iwe vigumu kuendelea na shughuli.” “Ingawa Global Counsel haina uhusiano wowote na Peter Mandelson leo, jukumu lake kama mwanzilishi mwenza na mwenendo wake, haswa wakati wa miaka yake ya mwanzo, vimeunda umbo lisilofutika jinsi Global Counsel inavyoonekana nje,” kampuni hiyo iliongeza.