Ushuru mpya kimataifa wa 10% uliopigiwa upatu na Rais wa Marekani Donald Trump, uliotangazwa baada ya Mahakama Kuu, siku ya Ijumaa, kubatilisha sehemu kubwa ya ushuru uliowekwa na kiongozi huyo, umeanza kutumika leo Jumanne.

Imechapishwa:

Dakika 3 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Ushuru huu mpya, ambao agizo la kiutendaji lilisainiwa siku ya Ijumaa, unalenga kuchukua nafasi ya ushuru uliopo usio na ubaguzi pamoja na ule ulioainishwa katika mikataba mbalimbali ya biashara iliyosainiwa tangu wakati huo na washirika wengi wakuu wa biashara wa nchi hiyo.

Hata hivyo, hauchukui nafasi ya ushuru unaoitwa wa kisekta, kuanzia 10% hadi 50% kwa viwanda kadhaa, kama vile shaba, magari, na mbao, ambavyo havikuathiriwa na uamuzi wa Mahakama Kuu wa kubatilisha sehemu kubwa ya ushuru uliowekwa na kiongozi huyo wa Republican tangu arejee ikulu ya White House.

Pia hautumiki kwa bidhaa za Canada na Mexico zinazoingizwa Marekani chini ya Mkataba wa Biashara Huria wa Amerika Kaskazini (USMCA).

Maafisa wa Forodha walitangaza kwamba ukusanyaji wa ushuru uliofutwa na Mahakama Kuu utakoma kuanzia Jumanne saa sita usiku saa za Washington, wakati ushuru mpya wa ziada utakapoanza kutumika. Pia walisema kwamba wataanza kukusanya ushuru mpya wa 10% mara moja.

Kwa kiwango hiki kipya, rais wa Marekani alitaja sheria ya mwaka 1974 inayomruhusu kusawazisha biashara kati ya Marekani na washirika wake wa kiuchumi wakati usawa mkubwa katika usawa wa malipo unajitokeza.

Ushuru huu unatarajiwa kuongeza kiwango cha wastani cha ushuru kinachotumika kwa bidhaa zinazoingia Marekani hadi 13.7%, ikilinganishwa na 16% kabla ya uamuzi wa Mahakama Kuu, kulingana na Maabara ya Bajeti ya Chuo Kikuu cha Yale.

Baada ya siku 150, serikali itahitaji kura kutoka kwa Bunge ikiwa inataka kudumisha ushuru huu kwa muda usiojulikana.

Siku ya Jumamosi, Donald Trump alisema kwamba alikusudia kuongeza ushuru hadi 15%, uamuzi aliouelezea ulitokana na “mapitio ya kina” ya uamuzi wa Mahakama Kuu, ambao kwa mara nyingine tena aliuona kuwa “wa kipuuzi” na “usio wa Kimarekani kwa njia isiyo ya kawaida.”

Hata hivyo, bado hajatoa agizo la kiutendaji kwa hilo.

Vikwazo vingine 

Agizo la kiutendaji kuhusu ushuru wa 10% linaanza kutumika hadi Julai 24, zaidi ya miezi mitatu kabla ya uchaguzi wa katikati ya muhula mnamo mwezi Novemba. Uchaguzi huu unaweza kupelekea Wademocrats wanapata tena udhibiti wa Baraza la Wawakilishi katika Bunge.

Ushuru huu unawezekana tu iwapo kutatokea usawa mkubwa katika urari wa malipo, ambao unajumuisha miamala yote ya kifedha kati ya nchi hizo mbili, ikiwa ni pamoja na biashara, mtiririko wa kifedha, na uwekezaji mtambuka.

Kwa hivyo, ingawa nakisi ya biashara ya Marekani katika bidhaa na Umoja wa Ulaya (EU) ilifikia dola bilioni 236 (euro bilioni 200) mwaka wa 2024, kulingana na data kutoka kwa Mwakilishi wa Biashara wa Ikulu ya Marekani (USTR), nakisi ya urari wa malipo ilikuwa takriban euro bilioni 70 (dola bilioni 82.5), kulingana na Tume ya Ulaya.

Ushuru uliofutwa siku ya Ijumaa na Mahakama Kuu ya Marekani ulitokana na sheria ya mwaka 1977 (IEEPA) inayoidhinisha serikali kuchukuwa hatua katika nyanja ya kiuchumi bila idhini ya awali ya bunge iwapo kutatokea “dharura ya kiuchumi,” ambapo majaji waligundua kuwa haijaonyeshwa.

Ushuru unaozungumziwa ulizidi dola bilioni 130 mwaka wa 2025, kulingana na wachambuzi.

Uamuzi huu unafungua njia ya marejesho ya ushuru ambayo tayari yamelipwa na makampuni. Kampuni ya usafirishaji wa vifurushi FedEx iliwasilisha kesi dhidi ya serikali siku ya Jumatatu.

Ushuru mpya uliyotangazwa mwezi Aprili, ulilenga nchi ambazo Marekani ilikuwa na nakisi ya biashara ya bidhaa, huku rais wa Marekani akiziona kama chombo cha kusawazisha biashara hiyo.

Lengo la Donald Trump pia lilikuwa kutoa mapato ya ziada kwa serikali ya shirikisho ili kupunguza makato ya kodi.

Hata hivyo, alibadilisha sehemu ya kozi hiyo kwa kuongeza misamaha kwa bidhaa kadhaa, hasa zile ambazo haziwezi kutengenezwa au kuzalishwa nchini Marekani.

Ushuru huu pia ulitumika kama msingi wa mazungumzo ya kusaini mikataba ya biashara na washirika wakuu wa Washington.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *