CRDB yaja na dhamana mbadala wachimbaji madiniCRDB yaja na dhamana mbadala wachimbaji madini

SERIKALI kupitia Tume ya Madini, Benki ya CRDB na wachimbaji wadogo wamesaini mpango maalumu wa mikopo kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu.

Wakati wa kusainiwa makubaliano hayo Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema mikopo hiyo imezingatia mambo mengi zikiwamo dhamana mbadala badala ya dhamana ya mali zisizohamishika.

“Huu ni muundo mpya wa kifedha unaotambua uhalisia wa sekta ya madini. Tumekubali dhamana zinazotokana na shughuli halisi za wachimbaji badala ya mali zisizohusiana na sekta. Hii itafungua milango kwa maelfu ya wachimbaji wadogo waliokuwa nje ya mfumo rasmi wa kifedha,” alieleza Nsekela.

SOMA: Tanzania yadhamiria kuwa kituo kikuu uchimbaji madini Afrika

Aliongeza: “Dhamana zitakazokuwa zinatumika ni leseni halali ya uchimbaji, mikataba ya mauzo, akiba ya dhahabu iliyohifadhiwa katika viwanda… hii ni uthibitisho benki imeamua kubuni suluhisho linaloendana na mazingira yaliyopo”.

Alieleza kuwa mbali na mikopo hiyo kuhusisha fedha za mitaji, lakini pia itahusisha mitambo na vifaa.

Alisema mpango huo utaleta mapinduzi katika uchimbaji mdogo na kufanya uwe wa kisasa, wenye tija na unaochangia kikamilifu uchumi.

“Sekta ya madini imeendelea kuwa nguzo muhimu ya uchumi lakini ukweli sehemu kubwa ya sekta hii imeshikiliwa na wachimbaji wadogo ambao ndio wengi… hata hivyo kwa muda mrefu wamekosa mitaji iliyo nafuu, teknolojia ya kisasa, wanakosa huduma za kifedha na ushauri wa kitaalamu ndio maana leo ni siku muhimu sana,” alifafanua Nsekela.

Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Ramadhan Lwamo alisema makubaliano hayo yataongeza mchango katika sekta ya madini na uchumi wa nchi kwa ujumla.

Waziri wa Madini, Antony Mavunde alisema mafanikio hayo ni matokeo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuonesha utashi na utayari wa kuikuza sekta ya madini.

“Tunachokishuhudia leo (jana) ni daraja linalounganisha maono ya serikali na nguvu ya mtaji kutoka sekta ya fedha. Ushirikiano huu unaenda moja kwa moja kumgusa mchimbaji mdogo na kumwinua katika uchumi rasmi. Benki ya CRDB hakika mmeonyesha kuwa ni benki kiongozi katika kuleta suluhisho stahiki kwa sekta mbalimbali. Tunawashukuru sana,” alisema Mavunde.

Aliongeza: “Wachimbaji mmekuwa nguzo muhimu sana katika uchumi wa Tanzania, nawathibitishia hatutawaacha tutawasimamia, tutawaendeleza nataka tuone wachimbaji wadogo mchango wao wa uchumi wa nchi ni mkubwa na jambo hili linawezekana”.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *