WAZIRI Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba ameendelea na ziara zinazoambatana na mikutano ya hadhara katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Arusha. Ziara hizo zilizoanza tangu Februari 13, mwaka huu zimeonesha taswira ya uongozi unaoshuka kwa wananchi, kusikiliza na kuchukua hatua.
Akiwa mkoani Tanga alikoanzia ziara, Waziri Mkuu ameonesha kwa vitendo kuwa uongozi si kukaa ofisini kusubiri taarifa, bali ni kwenda kwa wananchi kujionea hali halisi na kutoa uamuzi unaogusa maisha yao moja kwa moja.
Hii ndiyo njia inayopaswa kufuatwa na viongozi na watendaji wengine serikalini. Kiongozi anapokwenda kwenye miradi na kufanya mikutano ya hadhara, hupata picha halisi ya utekelezaji wa sera na matumizi ya fedha za umma.
Taarifa za mezani mara nyingi huficha uhalisia lakini sauti za wananchi hazifichiki. Ndiyo maana ziara za Dk Mwigulu zimekuwa na mvuto mkubwa kwa umma kwani zimegusa kero zao na kuibua matumaini mapya.
Mfano mahususi wa uongozi unaosikiliza ni agizo lake kwa Wizara ya Afya na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kukaa pamoja na kuwasilisha mapendekezo ya namna ya kupunguza gharama za matibabu.
Agizo hilo amelitoa baada ya wananchi kuwasilisha kero hiyo kwake. Gharama kubwa za matibabu ni eneo linalogusa maisha ya wananchi wengi hususani wenye kipato cha chini.
Kiongozi anapochukua hoja ya mwananchi na kuigeuza ajenda ya serikali, hujenga imani na kuimarisha mshikamano kati ya dola na watu wake.
Aidha, maelekezo yake kwa watendaji kuwa na jedwali linaloonesha kero zinazopokelewa na hatua zinazochukuliwa ni hatua ya kuimarisha utamaduni wa uwazi na ufuatiliaji.
Huu ni mfumo unaopunguza urasimu na kuongeza uwajibikaji. Wakati Rais Samia Suluhu Hassan alipomuapisha Dk Mwigulu kushika wadhifa huo, alimpa ujumbe mzito wa kusimamia utendaji wenye matokeo, uwajibikaji na mshikamano ndani ya serikali.
Kwa hiyo, ziara hizi ni utekelezaji wa moja kwa moja wa maelekezo hayo kwa kushuka kwa wananchi, kusikiliza na kuchukua hatua papo kwa hapo. Hii inathibitisha namna ambavyo Waziri Mkuu ameelewa dhamira ya Rais Samia ya kuwatumikia Watanzania kwa vitendo.
Zaidi ya yote, hatua hizi zinaakisi falsafa ya Rais Samia ya ‘Kazi na Utu’ kwani kazi inaonekana katika ukaguzi wa miradi, kubana watendaji na kusimamia matumizi sahihi ya rasilimali huku utu ukionekana katika kusikiliza kwa makini, kuheshimu maoni ya wananchi na kutafuta suluhisho la changamoto zao bila ubaguzi.
Viongozi na watendaji wengine hawana budi kufuata njia hii ili kuimarisha utumishi wa umma na kuleta maendeleo yenye tija na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.
