MECHI tatu za Ligi Kuu Bara zinatarajiwa kuchezwa leo Jumatano zikihusisha Yanga, Simba na Azam ambazo wikiendi iliyopita zilirejea katika mikiki ya ligi hiyo baada ya kuishia hatua ya makundi katika michuano ya kimataifa.

Aina ya timu zinazokwenda kukutana katika mechi za leo sambamba na tofauti ya pointi baina yao, inafanya kuwa na ushindani wa aina yake kwani kila moja inasaka ushindi utakaoiweka sehemu nzuri zaidi kwenye msimamo hali inayofanya kukaa kimtego.

Mbali na hilo, pia ushindani wa Yanga na Simba kuelekea Dabi ya Kariakoo wikiendi hii, unazidi kunogesha mechi zao za leo kwani kila moja inataka kuendeleza wimbi la ushindi ili Jumapili ziingie kwa kujiamini.

MECH 02

YANGA VS JKT TANZANIA

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga leo watakuwa wenyeji wa vinara wa ligi hiyo, JKT Tanzania kwenye Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge jijini Dar es Salaam kuanzia saa 10:00 jioni.

Tofauti ya pointi tatu baina ya timu hizi, unaifanya mechi hii kuwa na ushindani mkubwa kwani JKT Tanzania imepania kutokubali kushushwa kileleni na Yanga, huku Wanajangwani hao wanahitaji ushindi utakaoongeza mzuka kuelekea kuivaa Simba.

Rekodi za jumla zinaikaba JKT Tanzania kwani haijawahi kuifunga Yanga zilipokutana mara 10 kwenye ligi tangu msimu wa 2018-2019, ikipoteza saba huku ikiambulia sare tatu.

Katika misimu ya karibuni, JKT Tanzania imekuwa ikipambana isipoteze nyumbani, lakini ugenini imeshindwa kufanya hivyo.

Msimu uliopita timu hizo zilikutana mara tatu, mbili Ligi Kuu Bara na Yanga ilishinda nyumbani 2-0 na ile ya ugenini zikatoka 0-0.

Moja ilikuwa Kombe la Shirikisho (FA) hatua ya nusu fainali, Yanga ikashinda 2-0.

MECH 06

Katika mechi 10 za ligi baina ya timu hizo, yamepatikana mabao 21, huku Yanga ikifunga 18, JKT Tanzania ikipata matatu pekee. Ushindi wa mabao 5-0 ilioupata Yanga msimu wa 2023-2024, kinabaki kuwa kichapo kizito zaidi kukipokea JKT Tanzania kutoka kwa mpinzani wake huyo.

Kwa sasa, JKT Tanzania imeonekana kuwa na safu nzuri ya ulinzi ikiongozwa na beki wa kati Laurian Makame na katika mechi 16 ilizocheza, haijawahi kuruhusu mabao zaidi ya mawili, ikiambulia clean sheet tisa.

Safu hiyo ya ulinzi ya JKT Tanzania golini akiwepo Ramadhan Chalamanda, ina kazi ya ziada kuizuia Yanga ambayo ndiyo timu yenye safu bora zaidi ya ushambuliaji ikiwa imefunga mabao 22 katika mechi tisa ilizocheza, huku ikilinda vizuri nyavu zake zisitikiswe ikiruhusu mabao mawili pekee.

Hata hivyo, JKT Tanzania yenye mabao 18, Yanga inapaswa kuwa makini na nyota wawili wa kikosi cha maafande hao ambao ni Saleh Karabaka na Paul Pater wanaoongoza safu ya ushambuliaji wakifunga jumla ya mabao 11 kati ya 18. Karabaka anayo sita na Peter matano.

Rekodi ya kutopoteza mechi yoyote ya ligi, inaipa jeuri Yanga kuelekea mechi hii ambayo ikipata ushindi wa aina yoyote basi itakaa kileleni kwa tofauti mabao dhidi ya JKT Tanzania kwani hivi sasa Yanga ina pointi 25, JKT Tanzania inazo 28. 

Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves, amesema: “Vijana mpaka sasa wameonyesha kiwango kizuri, naamini kila mmoja anaridhishwa na kiwango na kesho (leo) tunaingia kwenye changamoto ya mechi na tupo tayari kukabiliana nayo.

“Kuhusu majeruhi, ninao wawili ambao ni wa muda mrefu kidogo, Khomein (Abubakar) hali yake ni ya tofauti sana ingawa naamini anaendelea vizuri. Mzize (Clement) alirejea mapema kutoka kwenye majeraha, uchunguzi wa madaktari unaonyesha anaendelea vizuri kwa sasa lakini sidhani kama atakuwepo katika mechi ijayo. Pia kuna Pacome (Zouzoua), Dube (Prince) Aziz (Andabwile) walikuwa majeruhi lakini leo (jana) tunakwenda kuwafanyia tathimini japo naamini wataungana na wenzao mazoezini. Ngoja tuone kwani tunahitaji kuwafanyia tathimini kwa kushirikiana na jopo la matabibu.”

MECH 05

DODOMA JIJI VS SIMBA

Saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Jamhuri uliopo Dodoma, wenyeji Dodoma Jiji wataikaribisha Simba, timu iliyotoka kuichapa Tanzania Prisons mabao 2-0 uwanjani hapo wikiendi iliyopita.

Simba iliyoachwa pointi tatu na watani zao wa jadi Yanga, inaingia kwenye mechi hii ikifahamu na Dodoma Jiji ni wanyonge kwao kutokana na rekodi zilivyo, lakini haipaswi kuchukulia hilo kwa mazoea kutokana na hali ilivyo msimu huu.

Dodoma Jiji yenye pointi 20 katika mechi 15 ilizocheza, inafahamu na ushindi katika mechi hii utaifanya kuishusha Simba iliyopo nafasi ya nne na pointi 22, kisha yenyewe kupaa hadi nafasi ya nne kutoka ya sita iliyopo sasa.

Msimu huu Dodoma Jiji chini ya Kocha Aman Josiah, imekuwa na rekodi nzuri uwanja wa nyumbani kwani mechi saba ilizocheza hapo imepoteza moja pekee ilipochapwa 3-0 na Pamba Jiji, huku ikishinda nne na sare mbili.

Simba katika ligi rekodi ya mechi za ugenini msimu huu ipo vizuri kwani imecheza tatu na kushinda zote dhidi ya JKT Tanzania (2-1), KMC (2-0) na Tanzania Prisons (2-0).

Mbali na hilo, katika mashindano yote msimu huu Simba tangu mara ya mwisho ifungwe 1-0 ugenini dhidi ya Esperance Januari 25, 2026 kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, imeshuka dimbani mara saba mfululizo bila ya kupoteza, hali inayoashiria ina mwendo mzuri.

MECH 03

Katika mechi hizo saba mfululizo ambazo Simba imecheza bila ya kupoteza, imezifunga Mashujaa (2-0), KMC (2-0) na Tanzania Prisons 2-0 (zote za Ligi Kuu). Pia ikashinda 1-0 dhidi ya Stade Malien katika Ligi ya Mabingwa na ushindi wa 3-0 mbele ya Greenland kunako Kombe la Shirikisho (FA), huku ikitoka sare dhidi ya Esperance (2-2) na Petro Atletico (1-1) zote za Ligi ya Mabingwa.

Katika misimu kumi ya Dodoma Jiji na Simba kukutana kwenye ligi tangu 2020-2021, Simba imeshinda mechi zote, hivyo huu ni mtihani kwa Dodoma Jiji kuhakikisha inafuta rekodi hiyo mbovu hasa inapokuwa nyumbani.

Mara ya mwisho, Simba iliiangushia Dodoma Jiji kichapo cha mabao 6-0 zilipokutana msimu uliopita Machi 14, 2025 jijini Dar, huku ikishuhudiwa msimu huo pia Dodoma Jiji ikifungwa 1-0 kwao, hivyo kupoteza kwa jumla ya mabao 7-0.

Hii itakuwa ni mechi ya mwisho kwa wachezaji wawili wa Simba, Jonathan Sowah na Allasane Kante kukosekana baada ya kutumikia adhabu ya kukosekana mechi tano mfululizo za Ligi Kuu Bara ambazo ni dhidi ya Mtibwa Sugar, Mashujaa, KMC, Tanzania Prisons na Dodoma Jiji, hivyo wataendelea kutumika dhidi ya Yanga, Machi Mosi mwaka huu.

Desemba 17, 2025, Sowah na Kante waliadhibiwa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kutokana na makosa ya utovu wa nidhamu waliyofanya dhidi ya Azam FC, katika mechi ya Desemba 7, 2025.

Akizungumzia mechi dhidi ya Dodoma Jiji, Kocha wa Simba, Steve Barker, amesema: “Tumejipanga vizuri, mpinzani wetu wa kesho (leo) ni mzuri, jambo zuri kwetu tumeanza kuonyesha matokeo mazuri ya mfululizo. Tunaendelea kujiimarisha katika kiwango cha utengenezaji nafasi na kuzitumia kupata ushindi. Mechi ya kesho (leo) itakuwa ngumu, lakini tayari tumejiandaa kukabiliana na hali yoyote.

“Timu bora kesho (leo) naamini ndiyo itapata matokeo mazuri, kwa upande wetu tunahitaji kuendelea kuimarika kiuchezaji na kupata ushindi, kila mechi inakuja na changamoto tofauti. Hatutarajii mechi nyepesi.”

MECH 01

AZAM VS MTIBWA SUGAR

Ni tofauti ya pointi mbili tu inazitenganisha Azam na Mtibwa Sugar katika msimamo wa Ligi Kuu Bara. Mtibwa inazo 21 katika nafasi ya tano ikicheza mechi 15, huku Azam inazo 19 ikikamata nafasi ya nane.

Azam nayo ipo katika rekodi ya timu ambayo haijapoteza mechi ya ligi msimu huu kama ilivyo kwa Yanga. Ni timu mbili pekee hadi sasa zimefanya hivyo.

Mechi kumi za mwisho katika ligi zilipokutana timu hizi, Azam imekuwa wababe kutokana na kushinda saba, sare ikiwa moja na Mtibwa ikishinda mbili.

MECH 04

Azam imeichapa Mtibwa mechi saba mfululizo kuanzia Aprili 9, 2021, huku mara ya mwisho Mtibwa kuifunga Azam ikiwa ni Oktoba 26, 2020 iliposhinda 1-0, kabla ya hapo ilishinda pia 1-0, Julai 15, 2020, zote zikifanyika nyumbani kwa Mtibwa.

Mtihani kwa Mtibwa ni kwamba, haijashinda mechi yoyote ya ugenini msimu huu katika ligi ikishuka dimbani mara sita, ikiambulia sare nne na kupoteza mbili. Leo ina kazi ya kufanya mbele ya Azam ambayo nyumbani imeshinda mechi tatu na sare tatu, haijapoteza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *